Eric Bailly akubali kuhamia Beşiktaş
BEKI wa Mashetani Wekundi, Manchester United, Eric Bailly amekubali uhamisho kwenda kusakata soka katika timu ya Beşiktaş ya Uturuki.
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, mwenye umri wa miaka 29 sio sehemu ya mipango ya Kocha wa United, Erik ten Hag na ametumikia Marseille kwa mkopo msimu uliopita.
Bailly alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha Jose Mourinho Juni 2016 wakati alipowasili United akitokea Villarreal ya Hispania.
Amecheza mechi 113 akiwa United akifunga bao 1 lakini amekuwa akikabiliana na majeraha.
Taarifa ya Besiktas imesema: “Klabu yetu imefikia makubaliano na Manchester United kwa ajili ya hatua ya mwisho ya uhamisho wa beki wa Ivory Coast, Eric Bailly. Tunamtakia Eric Bailly, ambaye tunaamini atatoa huduma muhimu kwa klabu yetu, mafanikio makubwa na jezi yetu, na kuiwasilisha kwa mashabiki kwa heshima yetu.”
Beşiktaş ina muda hadi Septemba 15 kumsajili kwenye kikosi chake.




