MAUAJI ya kutatanisha yanayowahusu watu wasio na hatia, wakazi masikini wanaolala kwenye vibaraza katika Jiji la Mumbai (zamani Bombay) yanaibuka na kuzua taharuki.
Watu hao wanauawa kwa kupondwa na mawe makubwa vichwani wakati wakiwa usingizini na muuaji ambaye hakuna anayemjua na wala hakuwahi kupatikana.
Muuaji huyu anayetisha katika filamu hii (kama ilivyokuwa kwa hali halisi) anajulikana kwa jina la ‘Stoneman’, jina analopewa na vyombo vya habari na inaonekana kuwa mauaji ya mtu wa tano yanashindwa kuwashawishi Polisi wa Mumbai.
Lakini kwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Sanjay Shelar, ambaye amesimamishwa kazi kwa kumpiga hadi kumuua mhuni mmoja aliyewekwa mahabusu, mauaji haya yanampa fursa
nzuri ya kufanya upelelezi ili aweze kurudi kazini.
Sanjay anapania kufuatilia nyendo za Stoneman ili kujihakikishia nafasi ya kurudi
kulitumikia tena Jeshi la Polisi. Pamoja na msaada wa siri anaoupata kutoka kwa mkuu wake wa kazi, AIG Satam, Sanjay anaanzisha mchakato mkali wa kufuatilia nyendo za Stoneman.
Katika kuhakikisha anafanikiwa, anaomba msaada kutoka kwa msaidizi na rafiki yake anayeitwa Kamble, lakini Kamble anamwambia Sanjay kuwa hataweza kumsaidia kwa kuwa ana tatizo la kukimbiwa na mkewe.
Hata hivyo, Sanjay anajikuta akiingia kwenye mzozo na mpelelezi mwenzake wa polisi anayeitwa Kedar Phadke, ambaye ndiye amekabidhiwa kushughulikia kesi hii. Wote wawili; Sanjay na Kedar kila mmoja kwa wakati wake, wanazama katika upelelezi wa kesi hii.
Sanjay anapania kuwa wa kwanza kumpata Stoneman kwa msaada wa mtoa habari wake anayeitwa Ghanshu, huku akitafuta sababu za kwa nini Stoneman anaua watu kwa mawe.
Katika uchunguzi wake, Sanjay anagundua kuwa Stoneman anaua watu masikini tu hasa wale wanaolala mitaani (ombaomba, vibarua, wafagiaji n.k).
Watu walio mitaani wanahisi kuwa huenda Stoneman ni dereva wa teksi nyakati za usiku
aitwaye Mohammed.
Kesi hii inamfanya mke ENOCK BELLA wa Sanjay anayeitwa Manali kukasirishwa na tabia ya mumewe kwa kuwa siku za karibuni ameonekana yupo ‘busy’ sana na mambo yake tu, na anadhani kuwa huenda mumewe ana uhusiano na mwanamke mwingine.
Usiku mmoja jiwe linarushwa na kuvunja kioo cha dirisha la nyumba ya Sanjay na kumfanya Manali adhani kuwa ni wavulana wa eneo hilo walikuwa wanacheza, lakini Sanjay anahisi kuwa aliyefanya hivyo ni Stoneman.
Usiku mwingine tena Stoneman anajaribu kumuua ombaomba mmoja ambaye anamkuta akiwa amelala kando ya barabara lakini ombaomba huyo anaokolewa na polisi wanaolinda eneo hilo wakiongozwa na mpelelezi Kedari.
Wakati hayo yanatokea Sanjay naye yupo eneo hilo akifuatilia kesi hii lakini hataki Polisi wamwone, na hivyo katika harakati za kutaka kujificha, mpelelezi Kedar anamwona wakati akiondoka na gari lake kutoka eneo hilo.
Sanjay anapoingia katika ofisi yake ya kufanyia uchunguzi wa kesi hii anagundua kuwa imetembelewa na Stoneman ambaye ameacha alama. Sanjay anahisi hatari inaweza kutokea kwa mkewe na kumwomba aondoke haraka na kwenda kijijini kwao, lakini mkewe anaonesha wasiwasi na kusita kukubaliana na jambo hilo.
Hata hivyo, Sanjay anakwenda katika kituo cha treni ili kumkatia tiketi mkewe na huko anakutana na Stoneman lakini kabla hajamkamata, mpelelezi Kedari na timu yake wanampiga risasi ya paja wakidhani kuwa yeye ndiye muuaji.
Sanjay anafanikiwa kuwatoroka Polisi na kurudi nyumbani kwake, na tukio hilo la kupigwa risasi linamleta karibu na mkewe ambaye anampatia huduma ya kwanza.
Lakini katika uchunguzi wake hasa kwa alichoshuhudia kituo cha treni, Sanjay anahisi kuwa Stoneman ni mmojawapo wa polisi, kwa kuwa alimwona akiwa amevaa viatu kama vya polisi wa kitengo cha kushughulikia uhalifu.
Pia anagundua kuwa Stoneman anatoka katika kabila ambalo hufanya ibada za kutoa kafara, hivyo anampigia simu Kamble, askari anayemwamini na kumwomba kwenda kumweleza habari hizi bosi wake AIG Satam pamoja na kumpatia ushahidi wa kesi.
Hapo ndipo Sanjay anapojikuta akiwa karibu zaidi na kifo chake mwenyewe, kwani yeye ndiye anatakiwa kuwa mtu wa tisa na wa mwisho katika mfululizo wa mauaji hayo yenye kutatanisha.
The Stoneman Murders ni sinema iliyojaa taharuki mwanzo mwisho na itakuacha mdomo wazi pindi ukiitazama na kugundua kuhusu siri iliyogubika mauaji haya ya kutatanisha…
Filamu hii iliyotoka mwaka 2009, imetokana na kisa cha kweli cha mfululizo wa mauaji yaliyochukua nafasi kwenye vichwa vya habari vya magazeti jijini Bombay (Mumbai ya sasa) katika miaka ya 1980.
Filamu hii imejaribu kutoa majibu ya maswali kadhaa kuhusu kesi ya mauaji hayo
yaliyotingisha jiji hilo la Bombay na baadaye huko Calcutta katika miaka hiyo. Ni filamu ya kwanza ndefu kuongozwa na Manish Gupta.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com



