LIGI Kuu msimu wa 2022/2023 ulihitimishwa hivi karibuni, ambapo Yanga ilitawazwa kuwa mabingwa mara mbili mfululizo wakishika taji la 29 katika historia yake.
Ulikuwa msimu wenye baraka kubwa kwa klabu hiyo ya Tanzania, ambayo imemaliza ligi ikijivunia mataji matatu yaani Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (FA).
Yanga sio tu timu iliyotamba katika michuano ya kitaifa bali hata iliweka rekodi nyingine ya kimataifa baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
SIRI
Siri ya mafanikio ya Yanga ni pale walipoamua kufanya mabadiliko katika uongozi ili kuendesha timu kisasa chini ya mdhamini mkuu, Ghalib Said Mohamed (GSM).
Ndio maana kila timu hiyo inapofanya vizuri katika mashindano yoyote mashabiki wa klabu hiyo kwa kutambua mchango wa mdhamini huyo wamekuwa wakiimba jina lake kukubali kile ambacho anakifanya katika kuiletea klabu hiyo maendeleo.
Kingine, Yanga iliamua kumuamini Rais kijana Hersi Said kwa kumpa majukumu makubwa licha ya kwamba hakuwa na uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania.
Uwepo wake ulileta dharau kwa baadhi ya wachambuzi wa soka na wadau wakisema yeye ni mtoto mdogo bado hajui soka la Tanzania lilivyo, lakini mashabiki na wanachama hawakuogopa hilo walimwamini na hatimaye akafanya kile ambacho wengi hawakukitegemea.
Hersi aliamua kuingiza vijana wengi katika uendeshaji wa soka, akawaondoa wale viongozi wote wakongwe ambao walikuwa na janjajanja nyingi na wengine wakiwa ni chanzo cha migogoro ya chini kwa chini.
Chini ya uongozi wake, akaamua kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wazuri ukiongozwa na mshambuliaji; Fiston Mayele, Djigui Diarra ambao wameonekana na lulu kubwa kwenye kikosi hicho na pengine huenda wakapata ofa katika klabu nyingine za Afrika baada ya kutajwa katika tetesi za usajili.
Uwepo wa kikosi kizuri hakika umesaidia kuleta ushindani mkubwa katika ligi hata wapinzani wanalikubali hilo japokuwa hawawezi kusema hadharani.
Ndio maana klabu moja ilinukuliwa ikisema hata wao wanataka kufanya usajili mkubwa msimu ujao utakaoleta ubingwa Afrika kwa sababu tayari wameona matunda ya Yanga jinsi ilivyokuwa makini kusajili na hatimaye kufanya vizuri mashindano ya Afrika kwa kufika fainali hatua ambayo haikufikiwa na timu yoyote katika kipindi cha miaka 30 iliyopita baada ya Simba kuwahi.
SIMBA
Simba katika misimu hii miwili haikuwa vizuri baada ya kujikuta ikimaliza bila taji lolote, lakini pia ikimaliza katika nafasi ya pili. Wekundu hao licha ya kwamba waliamua kuingia katika mfumo wa mabadiliko ya kuendesha timu yao kisasa bado kuna mambo wanayafanya kizamani.
Simba ilitegemewa kwamba ingefanya vizuri zaidi sio tu katika ligi bali michuano ya kimataifa kwa kufika hatua za juu kwa maana ya nusu fainali au hata fainali. Wamekuwa wakisingizia kuwa wamekutana na timu kubwa kuliko wao kwa kulinganisha takwimu sababu ambayo sio ya msingi.
Walichotakiwa kufanya kama ukishaitwa wewe ni timu kubwa lazima uoneshe ukubwa wako mbele ya wakubwa wengine. Kwa maana hiyo kwa zaidi ya misimu mitano kuishia hatua ya robo fainali ni kwamba wamefeli.
KILICHOWAGHARIMU
Pengine ni kwa sababu bado asilimia kubwa ya viongozi waliopo ndani ya kikosi hicho ni wale wa miaka ya nyuma. Je, kama huko nyuma walishindwa kwanini waendelee
kuaminiwa wakati hamna kitu kipya walicholeta kwenye timu hiyo.
Kingine, usajili wao umekuwa wa janjajanja. Simba ni timu kubwa lakini haielewi namna wanavyosajili. Wanatumia mfumo wa kizamani. Utashangaa mchezaji anatajwa kununuliwa kwa gharama ambazo ni kubwa lakini kiwango chake uwanjani ni aibu.
Hutokea kwa wachezaji wengi kushindwa kuendana na mfumo lakini wapo wachezaji waliowahi kusajiliwa lakini hawakucheza baadaye wakaachana nao. Hiyo inaonesha wazi ni janjajanja.
Pengine ndio maana mwekezaji wao, Mohamed Dewji amekuwa akilalamika mara kwa mara kuwa kuna watu ni sababu ya timu kutofanya vizuri na kutishia kuwataja.
Ipo haja kama kweli Simba wanataka kuendesha mfumo kisasa wajitathmini tena, waangalie kama kuna watu wanawaangusha sio mbaya kuwafyekelea mbali kutafuta watu watakaowaamini na kuleta mapinduzi ya kweli.
AZAM FC
Azam FC inatajwa ni timu ya kitajiri na kila msimu wanaongoza kwa kufanya usajili mkubwa lakini bado uendeshaji wao hakika haueleweki. Kwa mara nyingine tena unaweza
kusema wamefeli msimu huu kwa sababu hakuna taji lolote walilopata zaidi ya kubadili makocha kila wakati.
Wamezoeleka kumaliza nafasi ya tatu au ya nne na kimataifa ndio kabisa hawajawahi kufika popote.
CHANGAMOTO
Timu hiyo inatajwa kukabiliwa na mambo mengi na kwanza ni bosi kuingilia uendeshaji inaonesha wazi hawaamini aliowaweka. Bosi wa timu hiyo anaelezwa yuko karibu na baadhi ya wachezaji kiasi kwamba kuna wakati inaweza kuathiri kikosi.
Haikatazwi ipo kila mahali ila linapotokea jambo la kazi awe makini kwa kuwaacha kushiriki kikamilifu na wenzao kwenye mazoezi ya maandalizi ya timu.
Azam FC inatakiwa kusajili wachezaji ambao wataleta ushindani kwa timu kongwe za Simba na Yanga lakini pia, wakishindwa ligi basi nguvu zao wazifanye kimataifa ili pale wanapopata nafasi wawakilishe kweli kwa kufika hatua za juu. Sio vibaya kujifunza kwa waliofanikiwa.
SINGIDA
Singida Big Stars hakika imejitahidi sana ikitoka kupanda na kumaliza ligi katika nafasi nne za juu. Hayo ni mafanikio makubwa kwao na inatarajiwa itawakilisha pia vizuri kimataifa. Timu hiyo kwa sasa imeuzwa kwa Fountain Gates hivyo inatarajiwa itaendeleza ubora wake
msimu ujao.
NAMUNGO
Timu hii nayo ni kama imefeli kwa sababu tangu ilivyobahatisha msimu wa mwaka juzi kumaliza ligi katika kiwango cha juu na kushiriki michuano ya kimataifa bado haieleweki.
Imemaliza ligi katika nafasi ya tano bila kikombe chochote.
IHEFU
Ni miongoni mwa timu ambazo zimeleta ushindani mkubwa msimu huu tofauti na matarajio ya wengi. Walianza mzunguko wa kwanza kwa mwenendo wa kusuasua lakini walivyofanya mabadiliko ya kikosi kwa kusajili wachezaji hakika walionesha matunda na kumaliza katika
nafasi ya sita.
GEITA GOLD
Geita Gold FC imekuwa ikionesha ushindani lakini bado kiwango chao sio cha kutisha hasa msimu huu.
PRISONS
Prisons wana bahati kwa sababu walikuwa wako vibaya na nafasi za mwisho lakini wamepambana na kubaki salama. Timu hii inatakiwa kubadilika na kufanya usajili mzuri
ili kutoingia katika presha.
Wengine waliokuwa kwenye presha ni Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Coastal Union waliokuwa wanapanda na kushuka nafasi za katikati.




