Kwingineko

Messi apiga bao sekundi ya 79

NYOTA wa Argentina, Lionel Messi amefunga bao la haraka zaidi katika maisha yake ya soka alipoingia kambani sekunde ya 79 katika mechi ya kirafiki ya timu yake ya taifa dhidi ya Australia iliyopigwa China.

Messi ametupia bao hilo la kihistoria akiwa nje ya kumi na nane baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Enzo Fernandez.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Beijing Workers’ Sports Complex jijini Beijing, Argentina imeibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0.

Bao la pili limetupiwa kimyani na German Pezzella.

Messi anatarajiwa kujiunga na Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Marekani (MLS) wakati mkataba wake na Paris Saint-Germain utakapofikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.

Nahodha huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 35 aliiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia 2022 wakati wa fainali zilizofanyika Qatar ambapo katika mashindano hayo alifanikiwa kutupia kambani mabao saba.

 

Imeandaliwa na Alfred Lukonge.

 

Related Articles

Back to top button