Ukurasa pendwa kwa West Ham na David Moyes

KLABU ya West Ham United ‘Wagonga Nyundo’ ya jiji la London, England imeandika historia mpya kwenye klabu hiyo kwa kutwaa taji la kwanza baada ya miaka 43.
Wagonga Nyundo hao wamenyakuwa ubingwa wa ligi ya Europa Conference kwa kuwafunga Fiorentina ya Italia mabao 2-1 kwakati wa fainali iliyopigwa Prague, Jamhuri ya Czech.
Huo ulikuwa ni mchezo wa 1097 kwa kocha David Moyes wa West Ham ambapo hakuwa na taji lolote lakini ameshinda ubingwa wake wa kwanza.
Historia imeandikwa pia kwa mchezaji wa West Ham, Emerson Palmieri dos Santos kwa kuwa mchezaji wa kwanza kushinda mataji yote yanayosimamiwa na Muungano wa Vyama vya Soka barani Ulaya(UEFA) yaani Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi ya Europa, Ligi ya Europa Conference, Kombe la UEFA Super na Kombe la Euro 2020.
Ushindi wa West Ham umeifanya Fiorentina kuwa timu ya pili kutoka Italia kupoteza fainali baada ya Roma kupoteza fainali ya Ligi ya Europa.
Sasa Inter Milan pia ya Italia inatizamwa kama inaweza kukwepa jinamizi hilo la kupoteza fainali itakavaana na Manchester City katika fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya Juni 10 kwenye uwanja wa Ataturk Olympic uliopo mji mkuu wa UTURUKI, Istanbul.
Imeandaliwa na Antipas Kavishe