Ndejembi akubali kuwa mlezi wa mpira wa kikapu Tanzania

DAR ES SALAAM: MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amekubali kuwa mlezi wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini, akieleza kuwa anaupenda mchezo huo na kutamani kuuona ukipata umaarufu mkubwa kama ilivyo kwa soka.
Aidha, amewataka wasanii na wafanyabiashara nchini kuwekeza katika mchezo huo kwa kumiliki timu ili kuupa msisimko wa kuongeza ushindani kama ilivyo kwa soka huku akiwataja wasanii kama Alikiba na Harmonize kuwa miongoni mwa wanaoweza kutumia uishawishi wao kuendeleza mchezo kama alivyofanya Emanuel Mkono ‘Nahreel’ kwa timu ya Reel.
Ndejembi alitoa kauli hiyo wakati wa fainali za Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam kati ya Dar City dhidi ya Stein Warriors zilizofanyika jana usiku kwenye Uwanja wa IST, Masaki, akisema anaamini mpira wa kikapu unaweza kuvutia mashabiki wengi zaidi endapo wadau wataungana kuwekeza katika mchezo huo.
Amesema moja ya mambo yaliyomvutia katika mashindano hayo ni ushiriki wa timu za wanawake, akibainisha kuwa uwepo wa timu 17 za wanawake unaonesha kuongezeka kwa mwamko wa mchezo huo miongoni mwa wanawake.

“Nasema, Naupenda huu mchezo,” amesema Ndejembi, akieleza matarajio yake ya kuona mpira wa kikapu ukipata hamasa na mashabiki wengi kama ilivyo kwa timu za soka nchini.
Amesema ili kufikia lengo hilo, kunahitajika wadhamini zaidi, wafanyabiashara na wasanii kujitokeza kuwekeza katika timu za mpira wa kikapu, akitoa mfano wa namna uwekezaji unavyoweza kusaidia timu kukua na kufanya vizuri katika mashindano.
Alitaja mfano wa timu ya wanawake ya Reel, ambayo amesema imepata mafanikio baada ya kupata wadau wanaoiunga mkono, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau unaweza kuleta mabadiliko katika mchezo huo.
Kuhusu miundombinu, Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itafanya juhudi kuhakikisha mahitaji ya viwanja vya kisasa vya mpira wa kikapu yanapatiwa ufumbuzi.
Pia, ameishukuru menejimenti ya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) kwa kutoa uwanja kwa ajili ya fainali hizo, akisema hatua hiyo ni mchango muhimu katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wadhamini, wafanyabiashara, wasanii na wadau wengine ni muhimu katika kuupanua mchezo huo na kuuwezesha kuvutia washiriki na mashabiki wengi zaidi.




