Ibraah atangaza nyimbo 50 za albamu mpya

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Ibraah, ametangaza orodha ya nyimbo 50 zitakazopatikana katika albamu yake mpya iitwayo “1B: The Other Side of the Face”, akieleza kuwa kazi hiyo itakuwa na mchanganyiko wa ladha tofauti za muziki na simulizi zinazogusa maisha ya kila siku.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ibraah amesema albamu hiyo itabeba maudhui mbalimbali yanayohusu mapenzi, maumivu ya kuachwa, maisha ya kila siku pamoja na nyimbo za burudani zinazolenga kuwafikia mashabiki wa makundi tofauti.
Ibraa amefichua kuwa albamu hiyo itakuwa na ushirikiano wa wasanii mbalimbali, wakiwemo Phina, Chid Benz, King Kaka, Dully Sykes na Paato, pamoja na wasanii wengine watano.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuleta mitindo tofauti ya uimbaji na kuongeza utofauti wa kimuziki katika albamu hiyo, ambayo Ibraah ameielezea kuwa ni zaidi ya mkusanyiko wa nyimbo za kawaida.
Amesema kazi hiyo inalenga kuwapa mashabiki uzoefu wa kipekee wa kimuziki kupitia simulizi na hisia tofauti zinazojitokeza katika nyimbo zake.
Katika hatua nyingine, Ibraah amewashirikisha mashabiki wake katika kuitangaza albamu hiyo kwa kuwataka kuchagua nyimbo tatu zinazowavutia zaidi kutoka kwenye orodha ya nyimbo 50 alizoweka hadharani.
Hatua hiyo imewapa mashabiki nafasi ya kuonesha mapema nyimbo wanazozipendelea kabla ya kufurahia albamu hiyo, huku ikiongeza matarajio kuhusu aina ya kazi ambayo msanii huyo anajiandaa kuiwasilisha kwa wapenzi wa Bongo Fleva.




