Mastaa

Trisha Khalid apata kazi mpya, aungana na Dkt Ofweneke

NAIROBI: MWIGIZAJI, mwanamitindo na mtayarishaji wa maudhui nchini Kenya, Trisha Khalid, amepata nafasi mpya ya kuongoza kipindi cha televisheni cha Hello Mr. Right Kenya, baada ya kutangazwa kuwa mtangazaji mwenza wa msimu wa tano wa kipindi hicho.

Trisha atajiunga na mtangazaji Dkt. Ofweneke pamoja na mtaalamu wa masuala ya mahusiano, Gertrude Mungai, katika kipindi hicho kinachojikita katika mapenzi, mahusiano na changamoto zinazowakabili watu wanaotafuta wenza wa maisha.

Hatua hiyo inamfanya Trisha kuchukua nafasi iliyoachwa na Risper Faith, ambaye alikuwa mtangazaji mwenza katika msimu wa nne wa kipindi hicho.

Uteuzi wake umetangazwa baada ya wiki

kadhaa za minong’ono, vidokezo na mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mtu ambaye angechaguliwa kuungana na Dkt. Ofweneke katika msimu mpya.

Akizungumzia uteuzi huo, Dkt. Ofweneke alisema timu ya uzalishaji ilikuwa na majina ya watu takribani watano waliokuwa wakizingatiwa kabla ya kufikia uamuzi wa kumchagua Trisha.

Alieleza kuwa vigezo vilivyoangaliwa ni pamoja na haiba, uchangamfu, uhalisia, ubunifu na namna kila mmoja anavyotazama masuala ya mapenzi na ndoa. Aidha, mwonekano wa mgombea pia ulikuwa miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa.

“Tulikuwa na majina takribani matano mezani. Tuliangalia haiba, nguvu, uhalisia na ubunifu wa kila mmoja, mitazamo yao kuhusu mapenzi na ndoa, na bila shaka tuliangalia pia uzuri. Mwishowe, kila kitu kilielekeza kwa Trisha Khalid,” alisema Dkt. Ofweneke.

Aliongeza kuwa anaamini atafurahia kufanya kazi na Trisha katika msimu huo mpya.

Kwa upande wake, Trisha ameahidi kuleta burudani, uchangamfu na nguvu mpya katika kipindi hicho, huku akitania kuwa huenda akampa wakati mgumu mtangazaji mwenzake.

 

“Natarajia kuona nguvu zaidi na burudani zaidi kutoka kwetu sote wawili. Niko tayari kumchanganya kidogo,” alisema Trisha akimzungumzia Dkt. Ofweneke.

Related Articles

Back to top button