Kiswahili Kung’ara Paris: BAKITA yatoa wito wadau kujisajili

DAR ES SALAAM: BARAZA la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limewataka wadau wote wa Kiswahili wenye nia ya kushiriki katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili, litakalofanyika jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Aprili 27 hadi 30, 2026, kujisajili mapema ili kuwezesha maandalizi ya kongamano hilo.
Akizungumza, jijini Dar es Salaam, Mhariri Mkuu wa BAKITA, Richard Mtambi, amesema kuwa zoezi la usajili kwa washiriki litahitimishwa Januari 31, 2026, lengo likiwa ni kupata idadi kamili ya washiriki na kuanza maandalizi rasmi ya safari na shughuli za kongamano.
Mtambi amesema “Lengo kuu la kongamano hilo ni kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa lugha hiyo kutoka mataifa mbalimbali.
“Kongamano la Kiswahili sasa litafanyika kila mwaka. Mwaka jana lilifanyika nchini Cuba ambapo mwitikio ulikuwa mkubwa na hamasa ya washiriki ilikuwa ya kuridhisha.
Baadhi ya machapisho yaliyowasilishwa yanatumika hadi sasa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani. Mwaka huu tunakwenda Paris, Ufaransa,” amesema Mtambi.
Ameongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuwahusisha viongozi wa kitaifa kama wageni rasmi, pamoja na wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, biashara, uwekezaji na utamaduni.
“Kupitia kongamano hili, tunawaunganisha wajasiriamali kutoka nchi mbalimbali ili wakutane, kubadilishana uzoefu na kufanya makubaliano ya kibiashara.
Pia tunatangaza fursa za uwekezaji katika sekta za utalii, kilimo, viwanda, biashara na elimu, sambamba na kutangaza vivutio vya Tanzania kimataifa,” amesema.
Mtambi amesema ushiriki katika kongamano hilo ni wa mtu binafsi, ambapo BAKITA imeanzisha kiungo maalumu cha usajili kitakachotumiwa na washiriki kujaza taarifa zao.
Baada ya hapo, taarifa hizo zitachambuliwa na kuhakikiwa kabla ya washiriki kuwasiliana na BAKITA kwa ajili ya taratibu za safari na maandalizi kwa ujumla.
Amefafanua kuwa kongamano hilo litafanyika katika ukumbi wa UNESCO jijini Paris, unaoweza kuchukua washiriki kati ya 500 hadi 800 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Aidha, amesema BAKITA inaendelea kuhamasisha taasisi na wizara kuwalipia watumishi wao kushiriki kongamano hilo, huku kukiwa na mpango wa kuratibu masuala ya viza, tiketi za ndege za pamoja na gharama za mshiriki binafsi.
Hata hivyo, Mtambi amebainisha kuwa kila mshiriki atajigharamia malazi na nauli akiwa jijini Paris.




