Mastaa

Zuchu amshukuru Shamira kwa upendo wa dhati

“Wewe ni miongoni mwa watu wachache wanaonijali bila masharti”

DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva nchini, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, ameonesha hisia zake za dhati kwa rafiki yake Shamira, mke wa meneja wake, Kim Kyando akimtaja kuwa ni miongoni mwa watu wachache wanaomjali na kumpenda bila kutarajia faida yoyote.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Zuchu ameweka wazi namna Shamira alivyo mtu wa pekee katika maisha yake, akisisitiza kuwa amekuwa nguzo muhimu ya ushauri, upendo na msaada wa kweli.

Zuchu ameandika:“Maishani nimekuwa mtu wa kutoa mara nyingi, kujali wengine zaidi na kuwapa hata bila kupewa.Ila wewe ni mmoja kati ya watu wachache sana wanaonijali na kunipa bila ya kutaka faida wala rejesho lolote kutoka kwangu.”

Msanii huyo ameongeza kuwa Shamira amekuwa mshauri wa karibu, anayemkumbusha mambo muhimu anapojisahau na kumwambia ukweli hata pale ambapo haukuwa rahisi kuusikia.

Aidha, amebainisha kuwa urafiki wao haujajengwa juu ya umbea au maslahi binafsi, bali ushauri wenye tija na manufaa kwa pande zote.

“Naupenda sana urafiki wetu kwa sababu umekuwa na faida nyingi. Wewe ni mtu mwema, roho safi na mfano bora kwangu na kwa familia yetu,” ameongeza Zuchu.

Katika ujumbe huo wa hisia, Zuchu ametoa shukrani kwa Shamira kwa kumpenda bila masharti, kumkubali pamoja na mapungufu yake, kuwa bega la kumlilia, pamoja na kumsaidia bila kudai malipo.

Akihitimisha ujumbe wake, Zuchu alimtakia Shamira heri ya siku ya kuzaliwa, akimuombea mema na kutamka wazi upendo wake wa dhati.

“Wewe ni ndugu yangu. Nakupenda sana. Happy birthday Best Friend,” ameandika Zuchu.

Ujumbe huo umeibua hisia chanya kwa mashabiki na wadau wa muziki, wengi wakimsifu Zuchu kwa kuthamini urafiki na kuonesha shukrani kwa watu wanaomzunguka.

Je wewe unae rafiki yako anayekwambia ukweli hata usiotaka kuusikia?

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button