Dube: hatujakata tamaa, tutajaribu tena

RABAT: MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Prince Dube, amesema kikosi hicho hakitakata tamaa licha ya kuanza vibaya fainali za Afrika baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Misri katika mchezo wa kwanza wa Kundi B uliochezwa jana nchini Morocco.
Akizungumza kupitia ujumbe aliouandika baada ya mchezo huo, Dube alisema: “Imekuwa ni Mungu tangu siku ya kwanza, hatukati tamaa na tutajaribu tena wakati mwingine,” akionesha imani na matumaini kuelekea michezo ijayo ya kundi hilo.
Katika mchezo huo uliochezwa jana, Zimbabwe ilianza kwa kishindo baada ya Dube kuifungia timu yake bao la kuongoza kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Misri ilisawazisha kupitia Omar Marmoush kabla ya nahodha wao, Mohammed Salah, kufunga bao la pili na la ushindi.
Licha ya kupoteza mchezo huo wa ufunguzi, Zimbabwe imeonesha dalili za ushindani mkubwa, huku Prince Dube akibaki kuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho kinachopambana kusaka matokeo chanya katika michezo ijayo ya Kundi B.
Mchezo ujao Zimbabwe itacheza na Angola Desemba 26, mwaka huu kabla ya baadaye kuhitimisha kwa Afrika Kusini.




