EPL

Arteta aweka mtego kwa ‘mastraika’ Arsenal

LONDON: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema mshambuliaji wa klabu hiyo Gabriel Jesus ana uwezo wa kuwa mshambuliaji namba moja wa timu hiyo, baada ya kurejea uwanjani wiki hii kufuatia kuwa nje kwa miezi 11.

Mshambuliaji huyo raia wa Brazil, mwenye umri wa miaka 28, alicheza dakika zake za kwanza tangu Januari alipoumia goti, akiingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Club Brugge kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano.

Jesus atapambana kuwania namba hiyo dhidi ya Viktor Gyokeres pamoja na Kai Havertz, ambaye kwa sasa anaendelea kuuguza majeraha ya goti. Arteta pia ana wachezaji wengi ubora katika maeneo ya ushambuliaji akiwemo Bukayo Saka, Eberechi Eze, Gabriel Martinelli, Noni Madueke na Leandro Trossard.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mechi ya Jumamosi dhidi ya Wolves, Arteta aliulizwa kama anaamini Jesus anaweza kupigania kuwa mshambuliaji chaguo la kwanza.

“Ndiyo, mchezaji wa kiwango chake, aliyeipa timu hii mengi, na alivyokuja na nguvu alizoonyesha siku ile, lazima apiganie nafasi hiyo,” – alisema Arteta.

Aidha, alipuuzilia mbali dhana ya kumuuza mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City licha ya wingi wa vipaji alivyonavyo katika safu ya ushambuliaji.

“Gabriel bado ana mengi ya kuifanyia timu hii. Ameonesha hilo sekunde ya kwanza tu alipokuwa tayari kucheza, Amefanya kazi kubwa kurudi kwenye hali yake, na sasa lengo ni awe nasi na atoe mchango wake.” – ameongeza.

Related Articles

Back to top button