EPL

“Salaha kukaa benchi kunaashiria hakuna mkubwa Liverpool” – Van Dijk

LIVERPOOL: Nahodha wa mabingwa watetezi wa EPL Liverpool, Virgil van Dijk, amesema uamuzi wa kumuweka Mohamed Salah benchi katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu England ni ishara tosha kwamba hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba kikosini bila kuonyesha kiwango cha kutosha.

Winga huyo raia wa Misri, mwenye umri wa miaka 33, hakuingia kabisa uwanjani katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Ham United Jumapili, na alitokea benchi Jumatano usiku wakati Liverpool ikitoa sare ya 1-1 na Sunderland.

Salah, aliyesaini mkataba mpya wa miaka miwili mwezi Aprili, amefunga mabao matano katika mechi 19 za mashindano yote msimu huu kiwango kinachozidi kuibua maswali baada ya kushindwa kurejea katika ubora aliouonesha msimu uliopita wakati Liverpool ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo.

“Hicho ndicho kilichokuwepo muda wote. Hakuna mwenye nafasi ya kudumu kikosini. Kila mmoja anatakiwa kufanya vizuri ili kuipambania nafasi yake.” – Van Dijk alisema akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Sunderland.

Aliongeza kuwa kocha Arne Slot ana sababu za kufanya maamuzi hayo, na kila mtu ndani ya kikosi ananapaswa kuchukulia maamuzi hayo kwa mlengo Chanya na kutanguliza maslahi ya klabu.

“Mo ameendelea kuwa mchezaji mkubwa, na nina uhakika bado atakuwa sehemu muhimu ya kile tunachotaka kufanikisha,” – aliongeza Van Dijk.

Liverpool kwa sasa wanashika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 22 katika mechi 14, wakiachwa kwa pointi 11 na kinara wa ligi Arsenal. Hii ni licha ya klabu hiyo kutumia pauni milioni 446 kwenye usajili wa dirisha la majira ya kiangazi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button