Niffer aandika ujumbe mzito kwa vijana

DAR ES SALAAM: BAADA ya kuachiwa kwa msamaha, msanii maarufu wa mitandaoni Jenifer Jovini, ‘Niffer’, ametoa ujumbe mzito wenye kugusa hisia nyingi kupitia ukurasa wake wa Instagram, akiwashukuru wanaompenda na kuwaasa vijana kujifunza kupitia safari yake.
Katika ujumbe mrefu ameuandika, Niffer alianza kujieleza kwa unyenyekevu:
“Name: Jenifer .b. Jovin, age: 26 years, season completed: madrasa tul yusuf.”
Akiendelea, amesema hawezi kulipa wema wa kila mtu aliyemuombea na kumuunga mkono wakati akiwa gerezani, na kwamba shukrani za kweli zimemtoka moyoni:“Nifanye nini hata niwashukuru wote mridhike? Nionge nini niwafurahishe? Hakika hilo siliwezi, isipokuwa Allah subhanahu wa ta’ala.”
Amesema kipindi alichopitia kimemfundisha mengi kuhusu maisha, ikiwemo thamani ya watu aliokuwa nao wakati wa misukosuko, huku akiwashukuru familia, marafiki na mashabiki waliompa nguvu katika kipindi chake gerezani alichokiita “madrasa yusuf”.
“Kila mara nilikuwa nakumbuka maneno yenu mazuri ambayo yamenifanya niwe strong mpaka sasa. Dunia imenifundisha mengi sana kwa muda huu mfupi. Hakika Allah aliniandalia kipindi hiki kama funzo la maisha,” ameandika.
Aidha, Niffer amesema matumaini yake makubwa ni kuwa vijana wajifunze kupitia kilichompata ili kuepuka makosa yanayoweza kuwapeleka kwenye hali ngumu kama aliyopitia.
“Kwenda kwangu madrasa yusuf (gerezani) kutawasaidia vijana wengi sana. Sitamani mwende kule ikiwa mimi naweza kukuelekeza jambo ukaliepuka,” amesema.
Amehitimisha ujumbe wake kwa dua na kuwashukuru wote waliomuombea mema: “Namuomba sana Allah awape kila lililojema, awaepushe na chuki na hasad, awazidishie riziki zenu. Niffer si wa Watanzania tu, ni wa dunia nzima.”



