Wastara: Umaskini ni kitu kibaya na chakudhalilisha

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Wastara Juma, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kueleza kwa hisia kali namna umaskini unavyoweza kumdhalilisha mtu na kumfanya ajisikie kutengwa katika jamii.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Wastara ameandika ujumbe mrefu akieleza machungu anayoyaona au kuyashuhudia yanayoletwa na hali ngumu ya maisha.
Amesema kuwa licha ya watu kutopenda kuwa maskini, hali hiyo humfanya mtu akose heshima na hata kushindwa kushirikishwa kwenye mambo muhimu ya kifamilia.
“Umasikini kitu kibaya sana, kinadhalilisha sana japo hayupo anayetamani kuwa maskini.
“Hata ndugu zako wanaweza kukutenga na hupati taarifa zozote za kinachoendelea. Utasikia taarifa kutoka kwa jirani au mfanyakazi wa ndani. Lakini ukiwa na nacho, utashangaa nyumba inajaa, hujui hata wamefika wapi,” ameandika Wastara.
Akiendelea kueleza, Wastara alilinganisha umaskini na ugonjwa unaofanya watu wakukwepe.
“Hakuna anayependa umaskini, ni kama ugonjwa wa TB; ukiwa nao kila mtu anakukwepa. Kupitia hali hii ya kukosa ni ngumu sana, hasa unapohitaji vitu muhimu lakini huwezi kuvipata. Maumivu yanayokuja moyoni yanakufanya uhisi hata kuomba kifo bila kupenda,” ameongeza.
Ujumbe huo umewagusa watu mbalimbali mitandaoni, baadhi wakionyesha masikitiko yao na wengine wakitoa pole pamoja na ushauri kwa msanii huyo.




