Kwingineko

Emegha asimamishwa kwa ukosefu wa maadili

STRASBOURG: KLABU ya Strasbourg imemsimamisha nahodha na mshambuliaji wake, Emmanuel Emegha mchezo mmoja kutokana na kile ilichokitaja kama ‘kutoheshimu maadili, matarajio na kanuni za klabu.’

Katika tangazo la uamuzi huo lililotolewa leo Jumatano, Strasbourg haikufafanua undani ni tukio lipi hasa lililopelekea uamuzi huo lakini imesema kwamba mchezaji huyo atarejea kwenye kikosi kwa mchezo unaofuata.

“Tumechukua uamuzi huu kufuatia ukiukaji wa hivi karibuni wa maadili na kanuni za klabu, Emmanuel ni sehemu muhimu ya kikosi na daima amejitolea uwanjani. Atarejeshwa baada ya mchezo huu.” – imesema taarifa hiyo.

Strasbourg itasafiri kucheza dhidi ya Toulouse Jumamosi kwenye Ligue 1 kabla ya kuelekea Scotland kuivaa Aberdeen kwenye Europa Conference League Desemba 11.

Kwa mujibu wa gazeti la michezo la L’Équipe, hatua hiyo imechochewa na mahojiano ya hivi karibuni ya Emegha, ambaye pia ni nahodha wa timu. Mwezi uliopita, baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Lille, alidokeza kuwa huenda Strasbourg isingepoteza dhidi ya Monaco na Paris Saint-Germain iwapo angecheza mechi hizo.

Katika mahojiano mengine na chombo cha habari cha Uholanzi, mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Uholanzi alidai kuwa alidhani Strasbourg ipo Ujerumani alipokuwa akisaini kujiunga na klabu hiyo miaka miwili iliyopita.

Related Articles

Back to top button