Kwingineko

Monaco, Pafos ngoma ngumu

KOLOSSI: WABABE kutoka Ligue 1 AS Monaco wamebanwa mbavu ugenini dhidi ya Pafos ya Cyprus baada ya kupata sare ya mabao 2-2 katika Ligi ya Mabingwa Jumatano usiku, wenyeji wakipata bahati ya bao la kujifunga dakika za mwisho, wakitoka nyuma mara mbili na kuwanyima Wafaransa hao ushindi wa pili mfululizo ugenini.

Monaco, ambao walipata ushindi wao wa kwanza msimu huu dhidi ya Bodo/Glimt mchezo uliopita, sasa wako sawa na Pafos kwa pointi sita kwenye msimamo wa ligi. Timu zote mbili zimepata ushindi mmoja tu katika mechi zao tano hadi sasa.

Wageni walianza kwa kasi, Maghnes Akliouche akimlazimisha kipa wa Pafos kufanya kazi mapema kabla ya kufunga bao la ufunguzi katika dakika ya tano ya mchezo, akimpasia Takumi Minamino aliyeweka mpira wavuni kwa shuti la nje ya eneo la hatari.

Pafos walionesha uhai baadae, jaribio la Anderson Silva kutoka nje ya boksi likigonga mwamba kabla hawajapata bao la kusawazisha dakika ya 18 kupitia kichwa cha David Luiz kutoka karibu na eneo la penalti kufuatia mpira wa kona.

Makosa ya kipa wa Pafos yaliigharimu timu hiyo dakika nane baadaye baada ya pasi yake fupi kunaswa na Folarin Balogun, ambaye alipiga kombora safi lililorejesha uongozi kwa Monaco. Wafaransa walienda mapumziko wakiwa mbele baada ya kipindi cha kwanza kilichojaa kasi na misukosuko.

Kipindi cha pili hakikuwa na msisimko ule ule, na wakati ikionekana Monaco wangeondoka na pointi tatu, kichwa cha Ivan Sunjic kiligonga mwamba dakika ya 88 na mpira ukamgonga beki Mohammed Salisu na kuingia wavuni, na hivyo kuipa Pafos sare ya mwisho iliyookoa siku yao.

Related Articles

Back to top button