Lupita Nyong’o: Niliombwa mno niigize kama mtumwa

NEW YORK: MUIGIZAJI kutoka Mexico mwenye asili ya Kenya, Lupita Nyong’o ameweka wazi kuwa baada ya kushinda tuzo ya Oscar alipokea maombi mengi yakimtaka aigize kama mtumwa, jambo ambalo lilimshangaza na kumuumiza kiakili.
Muigizaji huyo mwenye miaka 42 alishinda Tuzo ya Academy ya Muigizaji Bora Msaidizi kwa uchezaji wake mahiri kama Patsey katika filamu ya 12 Years a Slave ya mwaka 2013.
Lupita anasema alitarajia mafanikio hayo yangemfungulia milango ya nafasi mpya na za uongozi katika filamu, lakini hakutarajia kupata ofa zinazofanana na filamu ile aliyocheza mwanzo.
Akizungumza kwenye kipindi cha CNN Inside Africa, alisema:
“Filamu ile ndiyo iliyoelekeza nafasi ya kila kitu. Lakini kilichonishangaza ni kwamba baada ya kushinda Oscar, nilitarajia nipate nafasi nyingi za kuongoza filamu. Badala yake, nilikuwa napewa ofa kama, ‘Lupita, tungependa ucheze filamu nyingine ya mtumwa, lakini safari hii uko kwenye meli ya watumwa.’ Hizo ndizo nafasi nilizopewa miezi michache baada ya kushinda tuzo yangu.”
Muigizaji huyo wa Black Panther alisema kipindi hicho kilikuwa cha hisia nyeti sana kwake, na alilazimika kupuuza makala na mjadala uliokuwa ukizunguka mustakabali wake Hollywood.
“Napenda kuwa mpiganaji mwenye furaha wa kubadilisha mitazamo kuhusu maana ya kuwa Mwafrika. Na kama inamaanisha nifanye kazi moja chache kwa mwaka ili nisiendeleze taswira zilizopitwa na wakati kuhusu watu wa bara langu, basi niko tayari kufanya hivyo.”




