Kwingineko

Advocaat atoa neno Curaçao kufuzu WC 2026

AMSTERDAM: KOCHA mkongwe Dick Advocaat amesema kufuzu kwa taifa dogo la Curaçao katika Kombe la Dunia ni “kitu cha ajabu zaidi” kuwahi kutokea katika maisha yake yote ya ukocha.

Kisiwa hicho cha Caribbean chenye idadi ya watu wasiozidi laki moja na nusu, ambacho ni sehemu ya Uholanzi kinachojitawala, kiliandika historia Jumanne mjini Kingston baada ya kupata sare dhidi ya Jamaica na kuwa taifa dogo zaidi kuwahi kufuzu Kombe la Dunia.

Advocaat, anayejulikana kwa jina la utani la “Little General”, amewahi kufundisha timu za mataifa nane tofauti na aliiongoza Uholanzi kufika nusu fainali ya Euro 2004 na robo fainali ya Kombe la Dunia 1994. Sasa atakuwa kocha mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

“Baada ya mchezo kama huu unataka kusema ni kitu kizuri zaidi kuwahi kunitokea, lakini nikifanya hivyo nawatendea haki vibaya matukio mengi niliyowahi kupitia,” Advocaat aliambia gazeti la Algemeen Dagblad katika maoni yake ya kwanza baada ya kutimia kwa ndoto hiyo.

“Hiki ndicho kitu cha ajabu zaidi kuwahi kufanya kama kocha. Ni jambo kubwa kwa kisiwa, na kwa wachezaji wetu ambao wametoka mbali.”

Advocaat alitazama mechi hiyo akiwa nyumbani The Hague usiku wa kuamkia Jumatano.
“Nimechoka kabisa baada ya mechi, zaidi kuliko ninapokuwa uwanjani. Unaweza kupanga kila kitu lakini unapoteza nguvu kabisa. Huu ulikuwa mchezo muhimu mno,” alisema.


Kocha huyo alikabidhiwa timu hiyo Januari mwaka jana na aliwahamasisha wachezaji wengi wenye asili ya Antilles wanaozaliwa Uholanzi kujiunga na timu ya taifa — hali iliyofanya kikosi kilichocheza dhidi ya Jamaica kuwa na wachezaji wote waliozaliwa Uholanzi.

“Tulienda kwenye sehemu za ajabu sana kwenye mechi za kufuzu, tukacheza kwenye viwanja vibaya kabisa. Nilikuwa nikiwaambia kila wakati, kila kitu kitategemea mechi ya mwisho na ndivyo ilivyokuwa. Lakini mwisho wa siku tumefika pale ambako vijana waliota, Kombe la Dunia nchini Marekani,” alisema.

Related Articles

Back to top button