Kwingineko

Dick Advocaat kuweka rekodi WC 2026

KINGSTON: KATIKA umri wa miaka 78, Dick Advocaat atakuwa kocha mwenye umri mkubwa zaidi kuongoza timu katika Kombe la Dunia (WC 2026) baada ya timu yake ya Curacao kulazimisha sare ya kusisimua dhidi ya Jamaica na kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye fainali za mashindano hayo.

Advocaat, ambaye amefundisha timu saba tofauti za taifa, ikiwemo vipindi vitatu akiongoza taifa lake la Uholanzi, na kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 1994, hata hivyo kufikisha Curacao kwenye Kombe la Dunia inaweza kuwa ni mafanikio yake makubwa zaidi.

Curacao Nchi ndogo ya kisiwa inayojitawala ambayo ni sehemu ya Uholanzi na yenye idadi ya watu zaidi ya 150,000 tu, ni taifa dogo zaidi kufuzu kwenye mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

 

Advocaat alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwezi Januari mwaka uliopita. Hata hivyo, alilazimika kuangalia timu yake ikifuzu akiwa mbali baada ya kuondoka mara tu walipowasili Jamaica mwishoni mwa wiki ili kurejea nyumbani The Hague kwa kile shirikisho la Curacao lilichosema kuwa ni “sababu za kifamilia.”

Kabla ya mchezo, Advocaat alisema kwenye taarifa: “Ni uamuzi mgumu sana kuwaacha vijana wangu hapa. Nililazimika kufanya uamuzi huu kwa moyo mzito, lakini familia ni muhimu zaidi kuliko soka. Kutoka Uholanzi, nitabaki nikiwa katika mawasiliano ya karibu na benchi la ufundi na nina imani kubwa na kikosi hiki.”

Vyombo vya habari vya Uholanzi vimeripoti kuwa saa 2 asubuhi Jumatano nchini Uholanzi wakati Advocaat aliketi kuangalia mchezo, akiwa na mawasiliano ya simu na meneja wa timu, Wouter Jansen, ambaye alipeleka maelekezo yake kwa makocha wasaidizi Dean Gorre na Cor Pot wakati wa mapumziko.

Curacao walijiona na bahati katika Uwanja wa Independence uliyojaa mashabiki wakati Jamaica ikigonga nguzo tatu katika kipindi cha pili, ingawa walipata nafasi zao na kumshughulisha Golikipa mzoefu wa Jamaica Andre Blake.

Hadithi ya ndoto ilionekana kuharibika dakika ya nne kati ya tano za muda wa nyongeza pale mchezaji wa Curacao, Jeremy Antonisse, alipomuangusha katika eneo la hatari kiungo wa kati wa Jamaica Isaac Hayden na mwamuzi raia wa El Salvador, Ivan Barton, kuamua mkwaju wa penalti.

Lakini referee huyo alihimizwa haraka na maafisa wa VAR kuangalia tukio hilo kwenye skrini ndogo kando ya uwanja na bila kusita alibadilisha uamuzi wake, jambo lililosababisha hasira miongoni mwa mashabiki wa Jamaica.

Furaha ya Curacao ilithibitishwa dakika chache baadaye wakati filimbi ya mwisho ilipolia kuashiria kuanza kwa sherehe zao, huku dunia ikisubiri hadi baadaye Jumatano kupata maoni ya Advocaat.

Awali Mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuiongoza timu katika Kombe la Dunia alikuwa Mjerumani Otto Rehhagel, aliyekuwa na umri wa miaka 71 na siku 317 alipofundisha Ugiriki katika mchezo wao wa mwisho wa kundi dhidi ya Argentina huko Afrika Kusini mwaka 2010.

Related Articles

Back to top button