Kwingineko

Mancini arudi Uarabuni

DOHA: KLABU ya Al Sadd ya Qatar imemtangaza rasmi Roberto Mancini, aliyewahi kuwa kocha wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, kuwa meneja wao mpya kwa mkataba wa misimu miwili na nusu.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 60 anarejea kwenye ukocha zaidi ya mwaka mmoja tangu aachane na kazi yake na timu ya taifa ya Saudi Arabia.

Mancini anachukua mikoba katika klabu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Qatar, ikiwa na pointi 14 baada ya michezo tisa, pointi nane nyuma ya vinara Al-Gharafa.

Kipindi chake cha mafanikio makubwa kilikuwa wakati akiwa Inter Milan, ambapo aliongoza klabu hiyo kutwaa mataji matatu ya Serie A, Kombe la Italia mara mbili, na Supercoppa Italiana mara mbili kati ya mwaka 2004 hadi 2008.

Aidha, Mancini aliiwezesha Italia kutwaa ubingwa wa Euro 2020, na aliiongoza Manchester City kutwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu ya England (EPL) msimu wa 2011–12.

Hivi karibuni, Mancini alihusishwa na uwezekano wa kuchukua mikoba ya Nottingham Forest kabla ya klabu hiyo ya EPL kumpa kazi Sean Dyche mwezi Oktoba.

Related Articles

Back to top button