Africa

Wachezaji Nigeria warejea mazoezini

RABAT: Wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria wameelekeza akili zao kikamilifu kwenye mechi ya Playoff ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Gabon kesho Alhamisi, baada ya kutatuliwa kwa mgogoro wa posho uliosababisha kugomea mazoezi.

Wachezaji wa Super Eagles waligoma kufanya mazoezi mapema Jumanne wiki hii wakitaka kulipwa malimbikizo ya posho na bonsai zao, ambazo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, zinadaiwa tangu mwaka 2019.

Kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X (zamani twitter), Nahodha wa kikosi hicho William Troost-Ekong amethibitisha kwamba suala hilo limepatiwa ufumbuzi, angalau kwa sasa.

“Suala limepatiwa suluhisho. Tupo pamoja na tumejikita tena kwenye michezo ijayo,” Troost-Ekong ameandika kwenye ukurasa wake wa X. Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) halijatoa kauli yoyote rasmi kuhusu makubaliano hayo.

Nigeria itachuana na Gabon katika nusu fainali ya playoff za Afrika mjini Rabat nchini Morocco, na mshindi atakutana na Cameroon au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika fainali itakayopigwa Jumapili.

Mshindi wa michezo hiyo atafuzu kushiriki mechi nyingine za playoff itakayoshirikisha timu kutoka mabara mengine mwezi Machi mwakani, ambapo mataifa mawili zaidi yataungana na mengine 46 kucheza Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button