Filamu

Adele afungua ukurasa mpya, kuja na hii

LONDON: MWANAMUZIKI wa Uingereza Adele Adkins, anatarajia kuingia katika uigizaji baada ya kuamua kubadilisha mkondo wa maisha yake ya muziki na kuingia kwenye tasnia ya filamu.

Kwa mara ya kwanza, Adele atajiingiza kwenye ulingo wa sinema kwa kuonekana kwenye filamu mpya inayotengenezwa na mbunifu wa mavazi Tom Ford. Filamu hii inajulikana kwa jina la ‘Cry to Heaven’, na itakuwa ni moja kati ya filamu zitakazoonesha vipaji vingi vya kimataifa.

Adele atajiunga na waigizaji wakubwa kama Nicholas Hoult, Aaron Taylor-Johnson, Colin Firth, Paul Bettany, na nyota chipukizi wa filamu Adolescence na Owen Cooper. Filamu hii imechukuliwa kutoka kwa kitabu cha Anne Rice kilichochapishwa mwaka wa 1982.

Tom Ford atakuwa muongozaji na mwandishi wa filamu hiyo. Hata hivyo, bado haijafahamika ni nafasi gani Adele na wenzake watacheza, lakini habari hiyo imethibitishwa na vyombo vya habari vya Marekani.

Hadithi ya kitabu kinachotumiwa kama mwongozo wa filamu inasimulia maisha ya wanamuziki wawili wa castrati waliovuma katika jiji la Venice, na jinsi maisha yao yanavyoshikana kwa undani.

Kando na Adele, waigizaji wengine walioshiriki ni Ciarán Hinds, George MacKay, Mark Strong, Hunter Schafer, na Thandiwe Newton.

Adele, ambaye ni moja ya nyota maarufu zaidi wa muziki wa Birtani, alitoka na albamu yake ya mwisho miaka minne iliyopita, na tangu aachane na makazi yake ya Vegas mwaka jana, amekuwa akijitenga na umaarufu wa shughuli za muziki.

Muongozaji wa filamu hiyo Tom Ford pia ameandaa filamu mbili zilizopata sifa kubwa ikiwemo ‘A Single Man; mwaka wa 2009 na ‘Nocturnal Animals’ ya mwaka wa 2016, ambayo imemletea tuzo za Bafta.

Mnamo 2022, Ford aliuza eneo lake la mavazi kwa kampuni ya Estee Lauder kwa dola bilioni 2.8 (£2.4bn), na baadae akatangaza kuwa atatamatisha safari yake katika tasnia ya mavazi na kuanza kuandaa filamu kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

“Nimefurahia sana kutengeneza filamu hizi mbili. Hizo ndizo nyakati za furaha zaidi nilizowahi kuwa nazo maishani mwangu,” alisema Ford kwenye mahojiano na GQ.

Related Articles

Back to top button