Kwingineko

Villarreal yaaibika Cyprus

KOLOSSI: TIMU ya Villarreal imeendelea na mwenendo mbaya katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupoteza kwa bao 1–0 ugenini dhidi ya Pafos Jumatano, huku beki Derrick Luckassen akifunga bao pekee lililoiwezesha timu hiyo ya Cyprus kupata ushindi wao wa kwanza katika michuano hiyo.

Ingawa Villarreal inafanya vizuri katika LaLiga kwa kushika nafasi ya tatu, hali ni tofauti kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa, ambapo sasa imekusanya pointi moja pekee, huku Pafos wakinyakua pointi tano hadi sasa.

Mchezo ulianza kwa kasi, wenyeji wakitengeneza nafasi ya mapema kupitia kwa kiungo Domingos Quina, ambaye alipiga shuti zuri lililopaa juu ya lango. Villarreal nayo ilipoteza nafasi kadhaa kupitia Ayoze Perez na Pape Gueye, ambao walishindwa kumalizia vyema nafasi muhimu.

Kichapo hicho kilianza mapema kipindi cha pili, baada ya Pafos kupata kona na Luckassen, aliyekuwa hana ulinzi wowote, akajitwisha na kupiga kichwa kilichojaa wavuni na kuwapa wenyeji uongozi.

Villarreal ilijaribu kusaka bao la kusawazisha, lakini juhudi zao zilionekana kukosa nguvu na mpango thabiti, hali iliyowaacha mashabiki waliojaa katika uwanja wa nyumbani wa Pafos Alphamega Stadium wakishangilia ushindi huo wa kihistoria.

Kwa kuzingatia mienendo ya klabu zote mbili kwenye UCL wadau wa soka hawakutarajia mabao mengi. Villarreal walikuwa wamefunga mabao mawili pekee katika mechi tatu zilizopita yote yakiwa ni katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Juventus huku Pafos walikuwa na bao moja pekee walilofunga kwenye kipigo cha 5-1 kutoka kwa Bayern Munich.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button