
CALIFORNIA: TASNIA ya filamu imempoteza mmoja wa waigizaji wake wakubwa, Diane Ladd, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 nyumbani kwake mjini Ojai, California.
Habari za kifo chake zimetangazwa na binti yake, Laura Dern, ambaye pia ni mwigizaji maarufu aliyeshinda tuzo za Oscar. Katika taarifa aliyoitoa kwa The Guardian, Laura alisema kwa uchungu:
“Nitakuwa na shukrani za milele kwa mama yangu. Alikuwa mwalimu, rafiki, na nuru katika maisha yangu.”
Mwaka 2019, Diane Ladd aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa mapafu unaoitwa ;idiopathic pulmonary fibrosis’, hali inayosababisha mapafu kushindwa kufanya kazi vizuri. Kwa mujibu wa mahojiano ya People Magazine mwaka 2023, madaktari walimwambia Laura Dern kuwa mama yake alikuwa na miezi sita tu ya kuishi.
Laura alikumbuka jinsi taarifa hiyo ilivyomvunja moyo: “Nilihisi kama dunia inaporomoka. Madaktari walituambia njia pekee ya kumsaidia ni kumfanya atembee ili apumue vizuri zaidi.”
Kwa kufuata ushauri huo, mama na binti walianza kutembea kila siku katika mitaa ya Santa Monica. Safari hizo za matembezi, zilizoanza kama tiba ya kimwili, ziligeuka kuwa chanzo cha ukaribu mkubwa wa kihisia kati yao.
Katika kipindi cha kupona kwake, Diane Ladd na Laura Dern walizungumza mambo mengi ya kibinafsi, ikiwemo maumivu ya zamani yaliyotokana na kifo cha dada yake Laura, aliyefariki akiwa na miezi 18 baada ya ajali ya kuzama majini.
Laura alieleza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa magumu sana, lakini yalileta uponyaji mkubwa kati yao:
“Nilitaka kumzungumzia dada yangu bila kumuumiza mama, bali kumsaidia kupona. Haikuwa rahisi, lakini ilibadilisha kabisa uhusiano wetu. Sasa naweza kumwambia kila kitu.”
Diane Ladd, ambaye aliteuliwa mara kadhaa kwa tuzo za Oscar, alijulikana kwa uigizaji wake mahiri katika filamu kama Chinatown, Alice Doesn’t Live Here Anymore, na Wild at Heart. Aliacha alama kubwa katika Hollywood kama msanii mwenye nguvu, roho ya huruma, na mama mwenye hekima nyingi.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa, si tu katika dunia ya filamu, bali pia katika maisha ya binti yake Laura Dern, ambaye kwa huzuni alisema:
“Kupitia maumivu yake, tulijifunza maana halisi ya upendo na msamaha.”




