Mtanzania kufanya kweli ‘Miss Earth’ Ufilipino

DAR ESALAAM: MREMBO wa Tanzania, Miss Amina Jigge, amepewa heshima ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano makubwa ya urembo duniani, Miss Earth 2025, yanayofanyika nchini Ufilipino.
Amina, ambaye kwa sasa yupo kambini na warembo wengine kutoka mataifa mbalimbali, ameonesha ari na dhamira ya kuipa Tanzania heshima katika jukwaa hilo la kimataifa.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, Miss Amina Jigge amewaomba Watanzania kumpa sapoti na dua, akisisitiza kuwa atatumia nafasi hiyo kutangaza utalii na utamaduni wa Tanzania.
“Ninajivunia kupeperusha bendera ya Taifa langu. Naomba Watanzania wote waniunge mkono katika safari hii muhimu,” amesema Amina.
Mashindano ya Miss Earth 2025 yanatarajiwa kuvutia warembo zaidi ya 90 kutoka mataifa mbalimbali, ambapo washiriki watapimwa si tu kwa urembo, bali pia kwa uelewa wao kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.



