Ligi Ya Wanawake

Karia: Ligi Kuu Wanawake Msimu huu itakuwa ngumu

DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake utakuwa na ushindani mkali zaidi, huku akizitaka taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini ligi hiyo ili kuinua soka la wanawake nchini.

Akizungumza mara baada ya mashindano ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake yaliyoshirikisha timu nne kubwa — Simba Queens, Yanga Princess, JKT Queens na Mashujaa Queens — Karia alisema kiwango kilichooneshwa na timu hizo ni ishara ya namna ligi itakavyokuwa ngumu msimu huu.

“Mtizamo wangu, Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu itakuwa ngumu sana. Tumeziona timu nne kwenye Ngao ya Jamii zilivyoonesha ushindani wa hali ya juu. Tunaamini hata zile ambazo hatukuziona nazo zimejiandaa vizuri,” alisema Karia.

Karia alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali kuwekeza katika ligi hiyo ili kusaidia timu ambazo bado hazina wadhamini wa uhakika, jambo ambalo limekuwa changamoto kwa baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo.

“Kuna timu chache tu ndizo zina wadhamini. Kukosa udhamini kunasababisha nyingine kupata shida kubwa kiutendaji. Tunaamini kama taasisi zikijitokeza kudhamini, ligi yetu itakuwa bora zaidi na itatoa ushindani mkubwa kimataifa,” alisisitiza Karia.

Aidha, Karia alizitakia kila la heri timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake katika maandalizi yao kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa ligi hiyo, akisema TFF itaendelea kuunga mkono jitihada za kuendeleza soka la wanawake nchini.

Ligi Kuu ya Wanawake inatarajiwa kuanza hivi karibuni, na tayari hamasa imeanza kuongezeka kufuatia ushindani ulioonekana katika mechi za Ngao ya Jamii, ambazo zilivuta mashabiki wengi na kutoa burudani ya kiwango cha juu.

Related Articles

Back to top button