
MCHAKATO wa kumpata Kocha Mkuu wa Azam unaendelea ambapo Kaimu Ofisa Habari wa timu hiyo Hasheem Ibwe amesema mpaka sasa makocha saba wazawa wametuma wasifu wao kuomba kazi hiyo.
Akizungumza na SpotiLeo Ibwe amesema milango ya kutuma maombi bado ipo wazi mpaka mwishoni mwa mwezi huu uongozi wa juu utakapoketi, kupitia maombi na kupitisha jina la mshindi.
“Kiujumla CV ambazo tumepokea mpaka sasa ni zaidi ya 110, uongozi utakuwa makini kumpata kocha ambaye atatimiza malengo yetu tuliyojiwekea,” amesema Ibwe.
Ofisa Habari huyo amesema malengo ya Azam ni kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na nje na hiyo ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika na miundombinu yake.
Kwa sasa Azam ipo chini ya kocha wa muda Kally Ongala ambaye tangu akabidhiwe mikoba baada ya Denis Levagne kuondoka amekuwa na mwenendo mzuri ikiwemo ushindi wa mechi nne mfululizo.
Inashika nafasi ya 2 katika msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara na pointi 26 sawa na Yanga inayoongoza zikitofautiana kwa mabao.