Masumbwi

Ramadhan Shauri: Nampepeche anakutana na mwamba

DAR ES SALAAM: Bondia mahiri wa ngumi za kulipwa nchini, Ramadhan Shauri, amesema mpinzani wake katika pambano lijalo, Issa Nampepeche kutoka Mwananyamala, anakutana na kazi ngumu, huku akisisitiza kuwa amejiandaa kwa kiwango cha juu na yuko tayari kutoa kipigo cha kihistoria.

Shauri alitoa kauli hiyo katika maandamano maalum ya kishujaa yaliyofanyika katika mtaa wa Banda, Mabibo jijini Dar es Salaam, kuelekea pambano la Dar Boxing Derby (Samia Calling Fight) litakalofanyika Julai 26, 2025 kwenye viwanja vya Leaders Club.

Maandamano hayo yaliibua hamasa kubwa kwa mashabiki wa mchezo huo waliomiminika kushuhudia mabondia wao wakijipanga kuelekea pambano hilo kubwa.

“Nampa tahadhari Nampepeche, ajue anakutana na mwamba. Sina masihara, nimejiandaa vya kutosha. Niko kwenye kiwango bora zaidi kwa sasa na pambano hili ni fursa ya kuonesha ubora wangu mbele ya mashabiki wa Dar es Salaam,” alisema Shauri kwa kujiamini.

Kwa upande wake, bondia Hassan Ndonga naye alionesha kujiamini kuelekea pambano lake kwa kusema kuwa atahakikisha anaibuka na ushindi wa kishindo kwa ajili ya mashabiki wake.

“Ninapigana kwa ajili ya watu wangu. Nataka kuhakikisha napiga kwa ustadi na kuwapa furaha mashabiki,” alisema.

Mbali na pambano kati ya Shauri na Nampepeche, mashabiki watashuhudia pia makabiliano ya mabondia wengine wakiwemo Nassibu Ramadhan atavaana na Ibrahim Class katika pambano la kulipiza kisasi, huku Loren Japhet akikabiliana na Said Bwanga wa Mbagala.

Khalil Kalama atapambana na Abdullazack Hamais, wakati Hamad Furahisha atazichapa na Japhet Herman. James Kibanzange naye atavaana na Ismail Boyka.

Kwa upande wa wanawake, pambano la kusisimua linatarajiwa kati ya Stumai Muki na Sara Alex, huku Debora Mwenda akikabiliana na Asia Meshack.

 

 

Related Articles

Back to top button