Echeverri kufunga kurasa CWC?

ATALANTA, Kiungo mshambuliaji wa Manchester City Claudio Echeverri huenda akakosa mechi zilizosalia za Kombe la Dunia la Klabu baada ya kinda huyo machachari kupata jeraha la kifundo cha mguu wakati wa ushindi wao wa 6-0 dhidi ya Al-Ain.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema kuna uwezekano mkubwa wa Echeverri akawa nje kwa wiki mbili au tatu huku akisema anasubiri taarifa rasmi ya madaktari kuthibitisha hilo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye miaka 19 alikuwa miongoni mwa wafungaji katika mchezo uliowahakikishia City nafasi katika 16 bora akifunga kwa ‘free kick’ iliyotinga moja kwa moja kambani lakini hawakuweza kuendelea na mchezo baada ya muda wa mapumziko kutokana na jeraha hilo
“Ana tatizo katika kifundo cha mguu. Nadhani atakuwa wiki mbili au tatu nje kwa bahati mbaya. Ninamhurumia sana, tunajihurumia sisi pia,” amesema Guardiola
Man City watakabiliana na Juventus katika mchezo wa mwisho wa kundi G wakiwa nafasi ya pili kwa pointi sita sawa na Juventus huku wakiwa na jukumu la kumaliza nafasi ya kwanza ya kundi hilo ili kukwepa kizaazaa kwani Mshindi wa pili wa kundi hilo anacheza na kinara wa Kundi H katika hatua ya 16 bora ambae kwa sasa ni Real Madrid