Kwingineko

Kolo Muani kanogewa na Juventus

WASHINGTON: Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa anayecheza kwa mkopo Juventus kutoka PSG Randal Kolo Muani amesema angependa kusalia klabuni hapo kwa msimu ujao baada ya mchezaji huyo kuonesha kiwango bora kwenye Mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia la Klabu ya jana Alhamisi.

Kolo Muani, ambaye aliwasili katika klabu hiyo akitokea Paris Saint Germain kwa mkataba wa mkopo wa muda mfupi mwezi Januari, aliifungia Juventus mabao mawili, Waitaliano hao wakiizamisha Al-Ain 5-0, na kufikisha mabao matano katika mechi sita za mwisho alizochezea klabu hiyo.

“Kusema kweli, ninajisikia vizuri sana hapa. Naweza kucheza vizuri na kufunga mabao. Nina furaha na natumai nitabaki,” kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 aliambia Mediaset baada ya mechi mjini Washington D.C.

Meneja mkuu wa Juventus Damien Comolli aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita kwamba Juventus walikuwa wanajadiliana mkopo mwingine na PSG wakati wakifanya mazungumzo ya kuongeza mkataba wa Kolo Muani kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu.

“Nina matumaini kwamba tunaweza kufikia makubaliano na PSG kuhusu mkopo kwa msimu mzima wa 2025/26 hawajafunga mlango wa mkopo, na wanajua mchezaji anataka kubaki nasi,” alisema.

Majibu ya kujiamini ya kocha wa Juventus Igor Tudor kufuatia ushindi wao wa Jumatano yanaweza kuwa yamechangiwa na ukweli kwamba wachezaji wawili waliofanya vizuri zaidi kwenye mchezo huo wako kwenye klabu hiyo kwa mikataba ambayo itaisha baada ya michuano hiyo.

Winga wa Ureno Francisco Conceicao, ambaye pia yuko kwa mkopo kutoka Porto, alifunga mabao mawili baada ya kuwatia gagaziko safu ya ulinzi ya Al-Ain kutoka pande zote mbili za uga wa Audi Field.

Tudor amemtumia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kwa uangalifu tangu achukue mikoba ya Thiago Motta mwezi Machi, akizingatia ukweli kwamba Juventus wanaweza wasiwe tayari kuvunja kipengele cha ununuzi cha euro milioni 30 kilichopo katika mkataba wake na kumbakisha Turin.

Hata hivyo Kwa muda huu mfupi Tudor anao wachezaji wote wawili wanaokiwasha kwenye Kombe la Dunia la Klabu, linaloendelea kwa Juventus na mechi dhidi ya Wydad Casablanca Jumapili na Manchester City Alhamisi ijayo.

Related Articles

Back to top button