Africa

Twiga Stars yatumia  CECAFA  kujinoa kwa WAFCON

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime amesema lengo lao kuu ni kuhakikisha wananyakua ubingwa wa mashindano ya CECAFA, lakini pia wanatumia michuano hiyo kama sehemu  muhimu la maandalizi kuelekea fainali za WAFCON zitakazofanyika baadaye mwaka huu.

Twiga Stars inatarajiwa kushuka dimbani leo Jumanne, Juni 17, kuikabili timu ya taifa ya wanawake ya Burundi katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya mashindano ya CECAFA yanayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Twiga Stars  ilianza mashindano hayo kwa kishindo kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0  dhidi ya Sudan Kusini.

Kocha Shime amesema wamejiandaa vizuri kwa kila mchezo na wamechukua mashindano haya kwa uzito mkubwa, wakilenga kutimiza malengo yao ya muda mfupi na mrefu.

Amesema  kila mchezaji anafahamu majukumu yake na amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa hii kuboresha mbinu na kuongeza uzoefu wa wachezaji kuelekea WAFCON.

“Kama tunavyojua siku zote mashindano ya CECAFA tunatumia kwa ajili ya kujiandaa kwa WAFCON, tunajaribu kila kile kinachowezekana kutusaidia katika maandalizi, lakini pia tunapambana kuhakikisha tunabeba kombe hili na kuliacha nyumbani,” amesema .

Shime ameongeza  kuwa kila mechi wanayocheza ni sehemu ya tathmini ya maendeleo ya kikosi chao, wameendelea kufanya marekebisho kwenye maeneo yenye changamoto, hasa safu ya ushambuliaji ambayo inalenga kuwa na ufanisi mkubwa zaidi katika mechi zinazofuata.

Related Articles

Back to top button