Ronaldo asitisha ubabe wa Wajerumani

MUNICH: NAHODHA wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameiongoza timu yake ya Taifa kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Ujerumani ndani ya miaka 25. Ronaldo mwenye miaka 40 alifunga bao lake la 137 wakati Ureno ikifanya ‘comeback’ na kulaza Ujerumani 2-1 mjini Munich katika nusu fainali ya UEFA Nations League usiku wa kuamkia leo.
Ushindi huo unakuwa wa kwanza kwa Ureno katika ardhi ya Ujerumani tangu mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia iliyopigwa katika mji wa Stuttgart Oktoba 1985 wakati huo ilikuwa miezi sita baada ya nyota huyo kuzaliwa mjini Madeira.
Katika mechi yake ya 220 kwenye rekodi, Ronaldo alikua mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga dhidi ya Ujerumani huku akimaliza ‘gundu’ lake. Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid alipoteza kila mechi kati ya tano za awali alizocheza dhidi ya Ujerumani.
Ureno haikuwahi kuifunga timu ya taifa ya Ujerumani tangu Kiuono wa zamani wat imu hiyo na kocha aliyepita wa AC Milan Sérgio Conceição alipofunga hat trick kwenye ushindi wa 3-0 kakika michuano ya Euro ya mwaka2000.
Katika mchezo huo, mtoto wa Sérgio Conceição, Francisco Conceição mwenye miaka 22 aliisawazishia Ureno dakika tano tu baada ya kuingia baada ya nyota anayetajwa kutua Liverpool Florian Wirtz kuitanguliza Ujerumani dakika ya 48 kabla ya Ronaldo kupeleka msiba kwa wajerumani mnamo dakika ya 68.
Ureno sasa iko fainali ikisubiri mshindi wa mtanange mwingine wa kukata na shoka wa nusu fainali nyingine ya Nations League kati ya Ufaransa na Spain huku ujerumani ikikodoa macho kwa atakaepoteza mchezo huo wawanie nafasi ya tatu.




