Filamu ya wasifu wa Michael Jackson yasogezwa mbele

NEW YORK:MPWA wa mwanamuziki ambaye ni marehemu Michael Jackson, Jaafar Jackson anatazamiwa kuigiza kama mwimbaji katika filamu ya ‘Michael’ ambayo inatarajiwa kutoka Aprili 1, 2026.
Awali kampuni inayosimamia uzalishaji wa filamu hiyo ya Lionsgate ilipanga kuizindua filamu hiyo Oktoba 3, mwaka huu wa 2025 lakini sasa imesogeza mbele uzinduzi wake hadi mwakani 2026 kwa sababu za kimazingira.
Filamu hiyo imeongozwa na muongozaji mashuhuri Antoine Fuqua na imetayarishwa na Graham King.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lionsgate Jon Feltheimer amesema:”Kuhusiana na wasifu wetu wa mwanamuziki Michael Jackson, tunafurahia saa tatu na nusu za wasifu wake katika filamu hiyo chini ya mtayarishaji Graham King na muongozaji mkuu Antoine Fuqua, na tutakuwa tukitangaza mkakati madhubuti wa kuitoa kwake wiki chache zijazo.
“Ningetambua kuwa kuna uwezekano tungeiachia ‘Michael’ katika mwaka wa fedha ambapo itaathiri matokeo ya kifedha ya ’26 lakini itaimarisha mfumo thabiti wa kifedha wa 2027.”
Upigaji picha wa ‘Michael’ ulifungwa Mei 2024, lakini hati, iliyoandikwa na John Logan, kwa sasa inafanyiwa marekebisho kabla ya upigaji picha upya kupangwa huku bajeti yake ikidaiwa kuwa dola milioni 155.
Mbali na Jaafar, waigizaji wengine katika filamu hiyo ni Colman Domingo mwenye umri wa miaka 54 na Nia Long mwenye umri wa miaka 53 kama wazazi wa Michael Jackson, Joe na Katherine Jackson.