United yanyoosha maelezo kwa Cunha

MANCHESTER:RIPOTI kutoka katika viunga vya Old Trafford jijini Manchester zinasema kuwa Mancheter united wako karibu kukamilisha ‘dili’ la mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Matheus Cunha baada ya kukubali kulipa dau la dola milioni 85 lililopo kwenye kipengele cha mkataba wake Wolves
Kituo cha televisheni cha BBC sport kimeripoti kuwa United sasa wako tayari kulipa dau hilo kwa awamu 3 ndani ya miaka miwili ijayo baada ya kukataliwa ombi lao la awali la kutaka kulipa kwa miaka mitano
United waliomaliza katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England msimu uliomalizika wako katika pilikapilika za kukiimarisha kikosi chao kabla ya kuanza kwa msimu mpya na uongozi wa klabu hiyo unaamini Cunha ni chaguo sahihi
Cunha mwenye miaka 26 alifunga mabao 17 msimu uliomalizika akiisaidia Wolves kuondoka kwenye vita ya kuepuka kushuka daraja, wakimaliza juu ya Manchester United kwa tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa
Hata hivyo Mbrazil huyo alishaonesha nia ya kuondoka Wolves akiliambia gazeti la The Guardian la nchini England mapema mwezi Machi kuwa anahitaji kuhamia kwenye klabu yenye ushindani zaidi na yenye nafasi nzuri ya kutwaa vikombe.