Ligi Kuu

Matola: Mchezo dhidi ya Singida leo hakutakuwa rahisi

DAR ES SALAAM:KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema kuwa mchezo wa leo dhidi ya Singida Black Stars hautakuwa mwepesi kutokana na ubora wa kikosi cha wapinzani wao.

Akizungumzia mchezo huo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam, Matola amesema kuwa licha ya Singida kuwa timu yenye ushindani mkubwa, Simba imejipanga kuhakikisha inapata ushindi na kuvuna pointi tatu muhimu.

Matola ameeleza kuwa baada ya kurejea kutoka katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane waliopoteza kwa jumla ya mabao 3-1, kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam na kuingia kambini kujiandaa kwa mchezo huu wa kiporo.

“Tunafahamu haitakuwa mechi rahisi, lakini wachezaji wetu wameelekeza mawazo yao katika mchezo huu. Tunaamini kwa maandalizi tuliyofanya, tuna nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri,” amesema.

Kwa upande wa wapinzani wao, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema kuwa malengo yao yamefanikiwa baada ya kufuzu kushiriki Kombe la Shirikisho la Afrika msimu ujao, lakini bado wanahitaji pointi tatu ili kumaliza msimu kwa heshima.

“Tunajua tunacheza dhidi ya timu yenye uzoefu wa kimataifa, lakini tumejiandaa vyema. Lengo letu ni kuonesha ushindani mkubwa na kupata matokeo mazuri,”amesema.

Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na malengo ya kila timu. Simba inahitaji ushindi kwenda sambamba na watani zao Yanga katika kuwania taji la Ligi Kuu hivyo presha inaweza kuwa kwao zaidi huku Singida ikiwa haina cha kupoteza ikisaka ushindi kwa ajili ya heshima tu.

Mchezo wa raundi ya kwanza Singida ikiwa kwao ilichapwa bao 1-0. Msimu uliopita Simba iliondoka na pointi nne kutoka kwa Singida mmoja wakipata sare ya bao 1-1 na mwingine walishinda 2-1.

Related Articles

Back to top button