Muziki

Taylor Swift kununua Rekodi zake za Muziki

MAREKANI: MWIMBAJI muziki wa Marekani, Taylor Swift, anaweza kupata nafasi nyingine ya kununua tena rekodi za awali za muziki wake ambazo zilichukuliwa kutoka mikononi mwake miaka kadhaa iliyopita.

Kwa muda mrefu, Swift amekuwa akijitahidi kurekodi upya albamu zake sita za mwanzo na kuzitoa kama matoleo ya kifahari yaliyopewa jina la Taylor’s Version.

Habari mpya kutoka Page Six zinaeleza kuwa mmiliki wa sasa wa rekodi hizo yuko tayari kuziuza. Cha kushangaza zaidi ni kwamba mmoja wa watu wanaoripotiwa kuhimiza dili hili ni Scooter Braun—mtu ambaye awali alinunua rekodi hizo kupitia kampuni ya Ithaca Holdings kabla ya kuziuza kwa Shamrock Capital kwa faida.

Hata hivyo, kwa mujibu wa DailyMail.com kuna mashaka kuhusu madai kwamba Braun anahamasisha mauzo hayo kwa Swift, zikieleza huenda ni juhudi za kusafisha jina lake baada ya kashfa na mgogoro wake mkubwa na Taylor.

Mwaka 2019, Taylor aliwahi kudai kuwa Braun alimtolea sharti la kusaini makubaliano ya kutofichua chochote (NDA) kabla ya kumweleza bei ya rekodi hizo. Swift alisema kuwa hata kama wangekosa kuelewana, bado angefungwa na mkataba huo na hangekuwa na uhuru wa kusema lolote dhidi yake.

Aidha, aliwahi kufichua kuwa alipojaribu kununua rekodi zake moja kwa moja kutoka kwa Big Machine, alielezwa kuwa angepewa rekodi moja baada ya nyingine kwa masharti kwamba aandae albamu mpya kwa kila rekodi ya zamani anayoinunua—mpango ambao ungeendelea kumfunga kwa lebo hiyo aliyotaka kuondoka.

Kwa sasa, chanzo kinasema kuwa Shamrock Capital inataka kuhakikisha kuwa Swift ana taarifa rasmi kuhusu nia yao ya kuuza rekodi hizo, kwani inawezekana hakuwahi kupewa fursa hiyo mara ya kwanza. Ikiwa dili hili litatimia, huenda Taylor Swift akapata haki kamili ya kazi zake za awali—jambo ambalo mashabiki wake wamekuwa wakilitamani kwa muda mrefu.

Related Articles

Back to top button