Kwingineko

Amorim aiganda United

BILBAO:KOCHA mkuu wa washindi wapili wa Europa League Manchester United, Ruben Amorim amesema na kusisitiza kuwa hatajiuzulu nafasi yake kama kocha wa klabu hiyo licha ya kelele za mashabiki kumtaka aondoke kufuatia mwenendo mbaya wa klabu hiyo msimu huu.

Kauli hiyo ya Amorim inafuatia klabu yake ya Manchester United kupoteza fainali ya Europa League kwa kufungwa bao 1-0 na Tottenham Hotspur, matokeo ambayo yameifanya timu hiyo kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao kwa sababu hata kwenye ligi ya nyumbani kwao England wanashika nafasi ya 16 na pointi 39 walizopata baada ya mechi 37 za ligi.

Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya Fainali hiyo ya usiku wa Jumatano, kocha Amorim amesema hatajiuzulu nafasi yake lakini yuko tayari kuondoka bila kudai fidia yoyote endapo bodi ya Manchester United itaona kuwa hafai kuendelea tena na kazi hiyo.

“Kama bodi na mashabiki wengi zaidi wataona sifai kuwa kocha, nitaondoka kesho (siku inayofuata) bila kudai fidia yoyote lakini sitaacha kazi kwa hiyari. Nina imani kubwa na kazi ninayofanya.”

Pamoja na hayo Amorim pia amekiri kuna changamoto kubwa ndani ya klabu hiyo na kwamba mabadiliko makubwa yanahitajika kuelekea msimu ujao akisisitiza anahitaji muda na imani kutoka kwa mashabiki ili kuleta mabadiliko chanya.

Related Articles

Back to top button