Frida Amani aeleza ndoto aliyoota kuwa uhalisia

DAR ES SALAAM:RAPA Frida Amani, amefunguka kwa hisia kuhusu hatua kubwa aliyofikia kwenye safari yake ya muziki akieleza namna ndoto aliyoita ya kufanya kazi na mwanamuziki mkongwe Lady Jaydee ilivyotimia.
Akizungumza na SpotiLeo Frida alisema ilikuwa kama ndoto kutamani kufanya kazi na msanii huyo wa muda mrefu na mwenye heshima kubwa, na siku moja aliona ndoto ikienda kuwa kweli baada ya Lady jaydee kumpigia simu na kutaka wafanye kazi Pamoja.
Frida Amani alieleza kuwa Lady Jaydee amekuwa chanzo kikubwa cha motisha tangu siku za mwanzo za safari yake ya muziki.
“Nimekuwa nikimtazama Lady Jaydee kama ‘inspiration’ kwa muda mrefu sana. Amefanya mambo makubwa sana. Mimi ananivutia kujitahidi ili niweze kufanikiwa kama yeye,” alisema Frida kwa msisimko.
Kwa miaka 25 kwenye tasnia ya muziki, Lady Jaydee amekuwa nembo ya mafanikio kwa wasanii wengi, na kwa Frida Amani, kufanya kazi naye ni zaidi ya muziki , ni ndoto iliyotimia.
“Nilikuwa sijioni kama wao, niliamini siku moja nitakuja kupata nafasi ya kufanya naye kazi ikawa ni ndoto. Alipokuja kunitafuta akaniambia ana ngoma yake anatamani tufanye kazi pamoja, sikuamini. Maana yake nimepambana kufanya kitu na Jide ameniona!”
Kwa Frida, mafanikio haya yanaonesha kuwa ndoto haziishii kuwa ndoto tu zikitunzwa na kufanyiwa kazi, hutimia. Amedokeza pia kuwa uzoefu wake wa kisanii umemfungulia milango mikubwa zaidi ikiwemo ya kimataifa.
“Kuna vitu una viota vinatokea. Kwa mfano, sikuwahi kuamini kama kuna siku nitakutana na Rais. Nimeota matamasha makubwa duniani na mengine nimekutana nayo. Nimekutana na Rais wa Finland na kupiga naye stori na hivi karibuni amekuwa mmoja wa wafuasi wangu katika mitandao yangu,”amesema.
Kazi aliyoshirikishwa Frida Amani na Lady Jaydee inaitwa Popo remix, wimbo ambao ulitoka wiki mbili zilizopita na unaendelea kufanya vizuri.




