Arsena yapanga Ubaya Ubwela Paris

LONDON:KOCHA mkuu wa washika mitutu wa jiji la London Arsenal, Mikel Arteta amesema wao kama timu wana ‘jambo maalum’ la kufanya jijini Paris katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani ulaya baada ya hapo jana kikosi chake kupotea kwa goli 1-0 goli la Ousmane Dembele mapema dakika ya nne tu.
Akizungumza baada ya mchezo huo Arteta amesema wana mlima mkubwa wa kupanda jijini paris lakini ni lazima kikosi chake kiwe na jambo maalum la kufanya ili kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali na kutimiza malengo yake ya kutwaa ubingwa wa UCL kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.
“Tupo kwenye half time, na ujumbe wangu kwa wachezaji umesalia ule ule. Tulishinda nyumbani 3-0 dhidi ya Real Madrid ni lazima twende Paris tukashinde mchezo tuna zaidi ya uwezo wa kufanya hivyo kwa sababu niliziona timu mbili bora sana na tofauti ya mabao ni ndogo (PSG) walikuwa wazuri mbele ya goli na golikipa wao alikuwa na kazi kubwa ya ulinzi”
“Tulifanya mambo mengi kwa usahihi sana, tulifanya vyema sana. Dakika za 15/20 zilikuwa zao walitushika wakapata bao la mapema walikuwa na muunganiko mzuri walitumia nafasi chache walizopata kutuadhibu. Tulikuwa na tatizo dakika hizo nashukuru tulirekebisha na tukauchukua mchezo. Kama unataka kushinda Champions League lazima uende Paris na misheni maalum” Amesema Arteta.
Arsenal wanapambana kuhakikisha msimu huu hawatoki patupu na sasa nguvu zao wamezielekeza kwenye UCL ambako wanatafuta kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza mbele yao ni kigingi PSG ambaye pia anatafuta kombe hilo kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.