Guardiola aapa kuipaisha tena Man City

MANCHESTER:KOCHA mkuu wa Manchester City Pep Guardiola ameapa kuirejesha timu hiyo kwenye ubora wake msimu ujao kufuatia kipindi kifupi kigumu kilichoikumba klabu hiyo kutokana na kile alichokiita kukosekana kwa ari ya upambanaji ndani ya kikosi hicho.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Nottingham Forest katika uwanja wa Wembley Jumapili Guardiola amesema aligundua kuanza kurejea kwa ari na umoja katika kikosi chake kwenye mchezo wa ligi walioshinda 2-1 dhidi ya Aston Villa jumanne na kusema kuwa hicho ni kitu kilichokosekana kikosini hapo kwa muda mrefu
“Tunajifunza kufanya bora zaidi, kutengeneza muunganiko mpya kwenye timu. tunavyoshangilia tukifunga goli, unajua Bernardo alipofunga goli la kwanza Jumanne tulishangilia wote, miili yetu ilizungumza furaha tuliokuwa nayo lakini pia ‘Passion’ ni jambo ambalo sijaliona kikosini kwa muda mrefu labda tangu Oktoba”
“Ni lazima turudishe ari tulokuwa nayo miaka tisa iliopita, msimu ujao tutakuwa bora kila mtu amejifunza, nadhani tutakuwa washindani wazuri wa taji la ligi kuu msimu ujao” – Amesema Guardiola
City wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi licha ya kuwa ndio mabingwa watetezi wakitwaa kombe hilo kwa miaka minne mfululizo. Wikiendi hii watawavaa Nottingham Forest kwenye nusu fainali ya kombe la FA na kipigo kwenye mechi hii kutamaanisha kuwa vigogo hao watatoka kapa msimu huu kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016-17.