Singida Black Stars yaweka bei kwa nyota wake wawili
Bilioni 6.6 zatajwa

SINGIDA:UONGOZI wa Singida Black Stars umeweka wazi kuwa thamani ya nyota wao wawili, Jonathan Sowah na Arthur Bada, ni jumla ya dola milioni 2.5 za Kimarekani (takribani Sh bilioni 6.6) kwa klabu yoyote inayowahitaji.
Hivi karibuni, kumekuwa na tetesi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wanawania kuwasajili wachezaji hao ili kuongeza nguvu katika kikosi chao kwa msimu ujao.
Msemaji wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema klabu yoyote inayomhitaji mshambuliaji wao, Jonathan Sowah, inapaswa kutoa dola milioni 1.5 za Kimarekani ( Sh bilioni 4).
Kwa upande wa Arthur Bada, Massanza ameweka wazi kuwa bado yupo kwenye mipango ya klabu hiyo, lakini endapo kuna timu inayomtaka, basi itahitajika kutoa dola milioni 1 za Kimarekani (Sh bilioni 2.6) ili kumsajili.
“Singida Black Stars bado tunamhitaji Bada kwa sababu tuna mipango naye, lakini kama kuna klabu inayomtaka, basi iwe tayari kulipa thamani yake ya dola milioni 1. Kwa Sowah, thamani yake ni dola milioni 1.5,” amesema Massanza.
Aidha, alisisitiza kuwa Singida Black Stars iko tayari kufanya biashara kwa masharti hayo, na chini ya hapo, klabu inayowahitaji wachezaji hao haina sababu ya kuwasumbua.
“Tunatamani waendelee kutumikia timu hii na kutusaidia kufanikisha malengo yetu kwa msimu huu,” ameongeza.




