“Natumai Jeraha lake si la muda mrefu” – Howe

BRIGHTON:KOCHA wa Newcastle United Eddie Howe yupo kwenye wasiwasi mkubwa juu ya upatikanaji wa mshambuliaji wake na mpachikaji mabao kinara wa kikosi hicho Alexander Isak katika mchezo wa kombe la FA dhidi ya Brighton Jumapili lakini anaamini majeraha yake sio ya muda mrefu.
Isak mwenye magoli 21 kwenye mashindano yote msimu huu hakuwa pia sehemu ya mchezo waliopoteza 2-0 mbele ya vinara wa Premier League Liverpool kutokana na jeraha la nyama za paja.
“Sijamuona tangu mchezo wa Liverpool, nadhani nitaangalia leo lakini sidhani kama ni tatizo la muda mrefu. Hatukuwa na cha kupoteza Jumatano na hatuna cha kupoteza kwa msimu ulipofikia lakini linapokuja Suala la ‘fitness’ kwa mchezaji tuna vingi vya kupoteza, tutaangalia hali yake leo kama yuko fit atacheza” amesema Howe.
Kuumia kwa Isak ni pigo kwa New Castle hasa wakati huu ambao ratiba ni ngumu inayojumuisha fainali ya kombe la Carabao dhidi ya Liverpool machi 16.
Vijana wa Howe ni wa sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya England pointi tatu nyuma ya Manchester City walio nafasi ya nne na bila shaka wangependa kuwa kwenye michuano ya Ulaya msimu ujao.