Echeverri: Aguero Alinishawishi Kuutua City

MANCHESTER: KIUNGO mshambuliaji mpya wa Manchester City Claudio Echeverri, amesema kuwa gwiji wa zamani wa klabu hiyo Sergio Aguero alimsaidia kufanya maamuzi ya kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England.
Echeverri, mwenye umri wa miaka 18, aliyesaini mkataba na Man City mwezi Januari, amesema katika mahojiano maalumu na klabu hiyo kwamba Aguero alikuwa kiungo muhimu kati yake na mabingwa hao wa England.
“Nilizungumza na Sergio, lakini pia nilizungumza na Martin Demichelis. Waliniambia kwa kina kuhusu ubora wa klabu hii iliyo na wachezaji wakubwa na historia nzuri. Nilipata kufahamu kwa undani uhusiano wa kipekee kati ya klabu hii na nchi yangu ya Argentina, hasa kupitia Sergio mwenyewe,” alisema.
“Aguero ni gwiji hapa Manchester City kwa kila alichofanya kwa klabu hii. Nilikuwa nikimtazama akicheza, na kwa kweli najisikia vizuri kuwa hapa,” aliongeza.
Echeverri anakuwa mchezaji wa 12 kutoka Argentina kuwatumikia matajiri hao wa jiji la Manchester; wengine ni Pablo Zabaleta, Carlos Tevez, Aguero, Willy Caballero, Nicolas Otamendi, Demichelis, Maximo Perrone na Julian Alvarez.