Featured

Nyambui: Nyerere aenziwe kwa kudumisha michezo

MSHINDI wa medali ya fedha wa michuano ya Olimpiki ya mwaka 1980, Seleman Nyambui, amesema wakati Tanzania inaadhimisha miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, wanahitaji kudumisha michezo shuleni.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Nyambui amesema enzi za Nyerere kiwango cha michezo kilikuwa juu kwenye shule na taasisi mbalimbali ambapo wengi waliokuwa wanatumikia timu za taifa walitoka kwenye shule za sekondari, vyuo vikuu, mashirika na
taasisi za Polisi na Jeshi.

Alisema uthamani wa michezo kwa miaka ya zamani ulisaidia kuibua vijana wengi wenye vipaji na hata ushiriki wa idadi ya wachezaji kwa mfano riadha kwenye michuano ya kimataifa ulikuwa mchezo mkubwa kitu kilichosaidia kupata washindi wengi.

“Nakumbuka michezo ilikuwa ya hali ya juu sana kuanzia shuleni hadi ngazi ya kitaifa, zamani tulikuwa tunafanya mashindano kwenye sikukuu za kitaifa kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu na yalikuwa yanagharamiwa na serikali, vyuo vyote vya ualimu walikuwa wanazalisha wachezaji, ilikuwa rahisi kupata wachezaji wazuri,” alisema.

Alisema kinachohitajika kwa sasa ili kufanya vizuri kwenye riadha na michezo mingine ubunifu unahitajika na idadi ya wachezaji iongezwe kwenye ushiriki wa kimataifa kama ilivyokuwa zamani walikuwa wanapeleka wanariadha 35-40 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola au Olimpiki.

Pia, alisema maofisa michezo, utamaduni, serikali na vyama vya michezo wanapaswa kushirikiana kuibua vipaji kwenye shule, vyuo kuanzia ngazi ya chini ikiwezekana taasisi na mashirika yarudi kuendeleza michezo.

Katika tukio ambalo Nyambui anamkumbuka Nyerere ni lile la mwaka 1972 alipokwenda
kwenye Uwanja wa Uhuru kushuhudia fainali za mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya riadha na kusema hakuna kitu kinachounganisha mataifa kama michezo.

Pia, alisema 1976 wakati Uwanja wa Amaan Zanzibar unazinduliwa, Nyerere alikwenda
kuwapa wachezaji bora zawadi walioshiriki mashindano tofauti ya kuanzia mwaka 1973, 1974 na yeye akiwa ni miongoni mwao na wanariadha wengine Filbert Bayi na Mwinga Mwanjala.

Alisema anakumbuka Nyerere alivyochukizwa baada ya kugundua zawadi alizopewa kuwapa wachezaji bora zilikuwa ni saa za ukutani na kamba za kuruka akisema hazikuwa na thamani.

Katika miaka ya 1970 hadi 1980, wanariadha kama Bayi, Juma Ikangaa, Nyambui walililetea taifa sifa kwa  kutwaa medali katika michezo mbalimbali kuanzia Jumuiya ya
Madola, All African games na Olimpiki.

Related Articles

Back to top button