Filamu

Dk Mapana afunguka kukua sanaa za maonesho

DAR ES SALAAM: Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk Kedmon Mapana, leo amekutana na viongozi wa Tanzania Bora Initiative, taasisi inayojulikana kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sanaa na uigizaji kupitia mchezo wao maarufu, Hii ni Africa.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na taasisi hiyo ili kuendelea kuinua sekta ya sanaa na kuboresha fursa za ajira kwa wasanii.

Dk Mapana amewapongeza viongozi wa Tanzania Bora Initiative kwa juhudi zao madhubuti za kuhamasisha vipaji, kuwajengea uwezo wasanii wachanga, na kutumia sanaa kama nyenzo ya maendeleo na mabadiliko chanya katika jamii.

“Sanaa ni nguvu kubwa ya kubadilisha maisha na kutoa ajira kwa vijana. Tanzania Bora Initiative imeonesha mfano mzuri wa jinsi sanaa inavyoweza kutumika kuleta maendeleo. BASATA ipo tayari kushirikiana nanyi ili kuhakikisha sekta hii inazidi kukua na kutambuliwa zaidi,” amesema Dk Mapana.

Kwa upande wao, viongozi wa Tanzania Bora Initiative walielezea dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano na BASATA, huku wakisisitiza kuwa sanaa si burudani pekee bali ni sekta yenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Mkutano huu unaashiria hatua nyingine muhimu katika kuhakikisha sanaa inapata msukumo unaostahili, ikiwapa wasanii nafasi ya kujikita zaidi katika kazi zao kwa ufanisi na ubunifu.

Related Articles

Back to top button