‘Simba tupo kwenye uangalizi mkali’

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema wapo chini ya uangalizi mkubwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA), hawatakiwi kufanya kosa lolote.
Amesema wamepewa kipindi cha miezi 12 baada ya adhabu yao ya kutoingiza mashabiki katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya CS Costantine Jumapili, Januari 19, Uwanja wa Benjamini Mkapa.
“Tuna kazi kubwa ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi letu, mechi muhimu kwetu licha ya kufuzu lakini tunahitaji kupata ushindi dhidi ya CS Costantine hapa nyumbani. Tunatambua tumezuiliwa kuingiza mashabiki uwanjani tukio la kuumiza sana na wengine kuwachanganya pakubwa.
“Adhabu hii ni mechi moja tukitumikia adhabu hii vizuri mechi ya robo fainali mashabiki wataingia uwanjani, hutakiwi kufanya kosa kama lile ikitokea tutafanya tena tutafungiwa mechi nyingine,” amesema.
Ahmed amewaomba wanasimba kuheshimu adhabu kwani wamepewa idadi maalum ya watu kuingia uwanjani, wamepokea utaratibu wa kuufanya kutoka CAF na kuufuata.
“Kumekuwa na maoni mengi watu wakitaka tuweke screen kubwa uwanja wa Uhuru ili kelele zitakazopigwa ziwafikie wachezaji, hairusiwi kukaa mita 1,000 kutoka uwanja jambo hilo haliwezekani na kufanya hivyo ni kuvunja sheria,” amesema.
Ahmed amesema Simba wanatambua mchango wa mashabiki na hivyo mdhamini wa michuano ya kimataifa amewaandalia eneo la Mwembe Yanga lililopo Temeke kuona timu yao.




