Azam FC yatangaza vita Simba, Yanga

DAR ES SALAAM: KLABU ya Azam FC imesema bado haijajitoa katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la Ligi Kuu itapambana na Simba, Yanga mpaka mwisho wa msimu kitaeleweka tu.
Akizungumza na SpotiLeo Dar es Salaam Msemaji wa Azam FC Hasheem Ibwe amesema kinachowapa jeuri ya kuamini wana nafasi ni uwezo wa kikosi chao hautofatiani sana na wapinzani wao wako tayari kupambana kufikisha malengo.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa pointi 36 katika michezo 16 nyuma ya Yanga yenye pointi 39 ikiwa nyuma mchezo mmoja sawa na kinara Simba yenye pointi 40 ikitofautiana pointi nne.
“Kuna mabadiliko yamefanyika kwenye kikosi chetu, timu inafanya vizuri na tumefanya maboresho machache tunaamini kwa uwezo wa kikosi chetu kama tutaendelea kuonesha kiwango bora mpaka mzunguko wa pili basi tutafikia malengo yetu ya kuchukua ubingwa kwa asilimia 100,” amesema.
Mara ya mwisho Azam FC kuchukua taji la Ligi Kuu ilikuwa msimu wa 2013/2014 tangu hapo haijachukua huku Simba na Yanga zikipokezana kwa zamu.
Azam FC ilikuwa na mpango wa kwenda kuweka kambi nje ya nchi baada ya ligi kusimama kupisha maandalizi ya fainali za Chan lakini baada ya kusogezwa mbele kwa michuano hiyo ya Afrika hadi Agosti uwezekano wa kwenda na mdogo.
Na hiyo ni baada ya Bodi ya Ligi Kuu kutangaza ligi itarejea wiki ya kwanza ya Februari badala ya Machi iliyopangwa awali.