“Gusa achia Kimataifa zaidi

DAR ES SALAAM: BAADA ya kufanikiwa kwa usemi wa Gusa achia twende kwao kwenye michezo ya Ligi Kuu, Yanga wameweka wazi kauli mbiu hiyo wanaihamishia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe.
Yanga wawakilishi pekee wa Tanzania katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa imeanza kupigia hesabu alama tatu dhidi ya TP Mazembe, katika mchezo utakaochezwa, Jumamosi, Januari 4, 2025, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema maandalizi yanaendelea, Kocha Sead Ramovic anafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita na ubora wa wapinzani.
“Tunaenda kufunga mwaka 2024 na kuanza 2025 na baraka kubwa. Mchezo dhidi ya TP Mazembe ni muhimu sana kwa sababu umeshika hatma yetu ya ligi ya mabingwa kucheza hatua inayofuata.
“Hatujapata matokeo mazuri katika michuano hii, baada ya kufanya vizuri ‘Gusa achia twende kwao’, kwa ligi ya nyumbani sasa inahamia Kimataifa ni zamu ya TP Mazembe,” alisema.
Kamwe amesema hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu katika kundi wanashika mkia na wanahitaji alama tatu za mchezo wa nyumbani kujiweka katika mazingira mazuri ya kutafuta nafasi ya kwenda robo fainali.
“Hii mechi sio ya Rais Hersi Said, wachezaji au wafanyakazi wa Yanga, bali ni mchezo wa Wanayanga wote kujitokeza kujaza Uwanja wa Benjamini Mkapa kusapoti timu yetu ikipambania alama tatu za kutafuta kucheza robo fainali,” amesema.