Kwingineko

Waliofanya vizuri 2024 walitunukiwa

DAR ES SALAAM: KILA msimu yanapomalizika mashindano yote kwa maana ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ndipo tuzo hutolewa kwa wachezaji wanaofanya vizuri katika vipengele tofauti zikigusa ligi ya wanawake, wanaume, waamuzi na watendaji mbalimbali.

Msimu huu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mabadiliko ya tarehe za utolewaji wa tuzo za msimu. Ilizoeleka kuwa tuzo hufanyika siku tatu baada ya kumalizika kwa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) au FA lakini msimu huu mambo yalikwenda tofauti.

TFF ilitangaza tuzo za msimu wa 2023/2024 zitatolewa wakati wa uzinduzi wa ngao ya jamii wa msimu wa 2024/2025.

Kwa bahati mbaya au nzuri tarehe hii kulikuwa na mwingiliano wa matukio. Kulikuwa na uzinduzi wa reli ya kisasa (SGR) ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alizindua treni mpya za kisasa na miundombinu ya treni ya kisasa (Standard Gauge).

Kanuni ya Ligi Kuu ya 11:11 inayohusu vikombe na tuzo inasema tuzo zinatakiwa zifanyike siku tatu baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Shirikisho la Azam.

Kubadilishwa kwa tarehe kulipokewa tofauti na wadau kwani wapo waliosema haipendezi kusogezwa mbele wakitaja sababu zao kuwa wachezaji wengi wanaweza kukosekana kwa kuuzwa klabu nyingine pengine nje ya nchi na wengine wakienda kwao wanaweza wasirudi kwa suala la mikataba na klabu zao.

Wengine walisema kusogezwa mbele kunaweza kupunguza mvuto wa sherehe yenyewe kwasababu sio wahusika wote watakuwepo.

Na baadhi walikubaliana na mabadiliko wakitegemea kuona mambo yakiendeshwa vizuri zaidi tofauti na huko nyuma.

Rais wa TFF Wallace Karia alieleza sababu za kusogeza mbele tuzo hizo kuwa walitaka kuboresha na kuwataka wadau watulie na hatimaye tuzo hizo zilitolewa mwezi Agosti mosi kama zilivyopangwa.

Tuzo hizo ziligawanyika katika makundi Matano. Tuzo za Kombe la Shirikisho za CRDB, Ligi Kuu ya Wanawake, Ligi Kuu NBC, Tuzo za Utawala na Tuzo za Ligi Nyingine. Hivi ndivyo maboresho yalifanyika.

Msimu huu kulikuwa na ongezeko la tuzo tatu ambazo hazikuwepo msimu uliopita na kati ya hizo tuzo mbli zilikuwa  mpya hazijawahi kutolewa, wakati tuzo moja iliwahi kutolewa lakini msimu uliopita haikuwepo. Tuzo mpya ni Mchezajl Bora wa Tanzania anayecheza Nje (Mwanaume) na Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje (Mwanamke). Tuzo nyingine ni Mchezaji Bora wa Soka la Ufukweni.

Zaidi ya wachezaji 20 waliofanya vizuri walikuwa wakiwania vipengele tofauti.

FURAHA

Furaha ya tuzo hizi ilikwenda Jangwani kwa Yanga ambao waliongoza kwa kuchukua tuzo nyingi kutokana na ubora wa kikosi chao kwa wakati huo.

Mshambuliaji wa Yanga Aziz Ki aliupiga mwingi kwa kuondoka na tuzo nne ambazo ni mchezaji bora wa Ligi Kuu, Kiungo bora, mfungaji bora mwenye mabao 21 na ya kikosi bora.

Kwenye tuzo za ufungaji bora kulikuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Feisal Salum ambaye alimaliza na mabao 19. Tofauti ya mabao mawili huku Waziri Junior akifunga mabao 12.

Aziz Ki alikuwa ni kivutio kwenye tuzo hizo hasa baada ya kujitokeza akiwa na rafiki yake mwanamitindo Hamisa Mobetto ambaye ni maarufu zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Kitendo cha kutokea kwake katika matukio kama hayo kilipendezesha kidogo ingawa kulikuwa na tafsiri nyingi kwa watu wa mpira.

Mbali na Aziz wengine ni beki bora Ibrahim Bacca, mfungaji bora shirikisho Clement Mzize, kipa bora wa shirikisho Djigui Diarra, Kocha bora Ligi Kuu Miguel Gamondi wakiwepo pia, kwenye kikosi bora sambamba na Mudathir Yahya, Dickson Job, Yao Kouassi na Maxi Nzengeli.

Kwa upande wa Simba waliopata tuzo ni beki Mohamed Hussein kwenye kikosi bora, Kocha Juma Mgunda na Azam FC kulikuwa na Feisal Salum, Kipre Junior ambaye pia alipata tuzo ya bao bora la msimu na Coastal Union Ley Matampi alishinda tuzo ya golikipa bora wa Ligi Kuu na Waziri Junior wa KMC kwenye kikosi bora.

Mshambuliaji wa klabu ya Paok ya Ugiriki, Mbwana Samatta alishinda tuzo ya Mchezaji bora wa kiume wa Tanzania anayecheza nje ya Tanzania huku Aisha Masaka akishinda mchezaji bora mwanamke anayecheza soka nje. Alikuwa anacheza BK Hacken ya Sweden na sasa upo Brighton ya Uingereza.Kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Aisha Mnuka wa Simba Queens alipata tuzo mbili ya mfungaji bora na mchezaji bora. Licha ya kuwa na msimu bora baadaye hakuonekana uwanjani kutokana na mgogoro wa kimaslahi kati yake na klabu yake.

Mchezaji Bora Ufukweni ni Jaruph Juma na jambo zuri kwake msimu huu amepata timu ya kucheza nchini Morocco akicheza soka la kulipwa la ufukweni ikiwa ni mara ya kwanza Tanzania kutoa mchezaji wa mchezo huo.

Kulikuwa na tuzo ya mchezaji Bora First League-Ayoub Masudi (African Sports),  Mchezaji Bora Championship  Edger William (KenGold), Mwamuzi Bora Bara  Ahmed Arajiga,  Mwamuzi Bora Wanawake  Amina Kyando, Mwamuzi Msaidizi Bara  Mohammed Mkono, Mwamuzi Msaidizi wanawake  Zawadi Yusuph, Tuzo za Rais TFF Said El Maamry, Tuzo ya Heshima  Leodger Tenga na Tuzo ya Heshima ligi ya wanawake ilitolewa kwa  Juma Bomba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa serikali Gerson Msigwa  alimpongeza Rais wa TFF Wallace Karia kwa mafanikio ya tuzo hizo akisema kila kitu kimeboreshwa.

“Ligi yetu leo inatazamwa kila pembe ya bara letu la Afrika na duniani kote, wachezaji wanapepea kila mahali, timu zetu zote tupo pazuri sana, tuwaombee TFF na viongozi, niwahakikishie serikali itaendelea kufanya kazi na ninyi,”alisema.

Katika hatua nyingine, kulikuwa na tuzo za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) zilifanyika Juni 9, mwaka huu kabla ya TFF.

Ni Yanga iliyoteka vichwa vya Habari kwa kushinda  tuzo ya Timu bora ya Kiume ya Mwaka 2023 kwa ngazi ya klabu.  Ndani ya mwaka huo Yanga ilitwaa Ubingwa Ligi Kuu, Ubingwa FA, Ngao ya Jamii sambamba na kufanikiwa kufika fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.

Timu ya taifa ya wanaume ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilishinda  tuzo ya Timu bora ya kiume Mwaka 2023 kwa ngazi ya taifa.

Washindi wengine wa tuzo hizo za BMT  2023 tuzo ya Mwandishi bora wa Michezo wa kiume Hussein Shafih wa Shirika la Utangazaji TBC,

Mwandishi bora wa Michezo wa kike ni Fatma Chikawe kutoka Azam Media, Ahmed Arajiga Mwamuzi bora wa kiume wa Mwaka tuzo na Mwamuzi bora wa kike wa Mwaka ni Pendo Njau.

Tuzo ya mwanamichezo bora chipukizi wa kiume ilikwenda kwa Romeo ambaye ni mkali wa kuogolea, mwanamichezo bora wa kiume mwaka 2023 ni bondia Yusuph Changalawe.

Tuzo ya Timu Bora ya klabu kwa upande wa wanawake, ilikuwa JKT Queens. Mwanamichezo bora wa kike mwaka 2023 ni bondia  Grace Mwakamele.

Timu ya Taifa ya Wanawake upande wa kriketi ilitwaa tuzo ya Timu Bora ya Taifa upande wa Wanawake, Vosta Isaya alipokea tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka kwa wenye ulemavu.

Tuzo ya heshima kwa nahodha wa zamani wa Taifa Stars ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Tenga.

BMT ilitambua hadi vipaji vya shule kwa kutoa tuzo kwa wanamichezo bora wa kike kutoka shuleni ni Happiness Fabian kutoka Kapuya Sekondari, Kaliua Tabora na mwanamichezo bora wa kiume kutoka shuleni ilikwenda kwa Agape Mwenda.

Related Articles

Back to top button